Tumepiga hatua kutimiza haki za binadamu Tanzania baada ya COVID-19: Sedoyeka 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka Tanzania, Profesa Eliamani Sedoyeka (katikati) akiwa na ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa 51 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu. Kulia kwake ni Naibu Mwakilishi wa Tanzania kwenye ofisi
UN News
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka Tanzania, Profesa Eliamani Sedoyeka (katikati) akiwa na ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa 51 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu. Kulia kwake ni Naibu Mwakilishi wa Tanzania kwenye ofisi za UN Geneva, Uswisi Balozi Hoyce Temu.

Tumepiga hatua kutimiza haki za binadamu Tanzania baada ya COVID-19: Sedoyeka 

Haki za binadamu

Mkutano wa   51 Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaendelea  mjini Geneva Uswis ukiangazia mada mbalimbali zihusuzo haki za msingi za binadamu zikiwemo haki za maendeleo na umewaleta pamoja nchi wanachama wa Baraza hilo. Na Tanzania kama mmoja wa wajumbe wa kudumu wa baraza hilo inahudhuria mkutano huo.  
 

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo unaongozwa na Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Profesa Eliamani Sedoyeka ambaye anafafanua ajenda za msingi wanazojadili na nafasi ya taifa lake mkutanoni.

Ametaja ajenda hizo kuwa ni pamoja na afya, barabara, huduma za kijamii, shule, hususan kuangalia yale makundi maalum kama watoto, akina mama na watu wenye umri mkubwa. 

Profesa Sadoyeka amesema, “sasa sisi Tanzania kama mjumbe wa kudumu tuko hapa kushiriki katika kutoa matamko mbalimbali ya kitaifa kuhusiana na mada zinazoongelewa lakini vilevile inapobidi kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali ambayo tumetajwa ili kujenga uelewa wa pamoja kwa sisi kama wanachama.” 

Alipoulizwa iwapo Tanzania imeshatoa tamko lolote, Profesa Sadoyeka amesema tayari wametoa matamko matatu ambayo kwa ujumla  yamezungumzia jinsi ambavyo taifa hilola Afrika Mashariki limejiandaa baada ya COVID-19 hasa kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi.

Amefafanua kuwa katika suala hilo wamezungumzia jinsi ambavyo serikali imepambana kujenga kwa mfano zaidi ya madarasa 15,000, kupeleka zaidi ya dola milioni 200 katika huduma za afya na kadhalika.

Vilevile wametoa matamko yaliyozungumzia uhuru wa nchi kuweza kujipangia mambo yake na kuweza kusimamia misingi ya utawala bora na  haki za binadamu kimataifa, lakini kila nchi ina uhuru wa kufuata kabita yake na kujipanga kama nchi. 

Profesa Sadoyeka amesema akiwa anawakilisha Wizara ya Maliasili na Utalii, mkutano huu unatoa fursa kubwa kwao kwani, “uwepo wetu hapa tunaangalia jinsi gani tutatangaza nchi yetu katika nchi za maeneo haya Uswisi , Ujerumani na nchi zinazozunguka hapa , lakini vile vile kuvutia wawekezaji kutoka upande huu kuweza kuja Tanzania kuwekeza katika maeneo ya kimkakati hususan katika utalii katila vile vivutio vyetu vikubwa vya utalii.” 

Kikao hicho kilichoanza Septemba 12 kinatarajiwa kufunga pazia tarehe 07 mwezi ujao wa Oktoba.