Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miongozo ya utalii imetuwezesha kushinda tuzo na utalii umerejea Tanzania – TTB

Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.
TTB Video screenshot
Afisa wa mbuga ya taifa nchini Tanzania akipima joto la mtalii kama moja ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.

Miongozo ya utalii imetuwezesha kushinda tuzo na utalii umerejea Tanzania – TTB

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 likiendelea kusababisha zahma kwingineko duniani na hata kukwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii, nchini Tanzania hali ni tofauti na kutokana na kuzingatia kanuni za kulinda wananchi na watalii, shughuli za utalii zimerejea na hata taifa hilo la Afrika Mashariki limepata tuzo ya Mhuri wa kimataifa. 

Akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC jijini Dar es salaam nchini humo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, TTB, Devotha Mdachi amesema  mhuri huo ni kutoka Baraza la Utalii na Usafiri lenye makao  yake makuu nchini Uingereza, “sababu iliyosababisha ni kwamba Baraza hilo limekuwa likitafiti na kuangalia ni nchi gani ambayo imeweka miongozo na inatekeleza miongozo kuhaikisha kwamba raia wake na wageni wanaotembelea nchi hizo wako salama. Tanzania tangu mwezi Juni mwaka huu tulizindua muongozo ambao unatumika na kampuni za utalii zilizoko hapa nchini na taasisi zinazohusika na utalii.” 

Ziara zinazofanyika kwa kutumia maputo kwenye moja ya mbuga za wanyama nchini Tanzania.
TTB Video screenshot
Ziara zinazofanyika kwa kutumia maputo kwenye moja ya mbuga za wanyama nchini Tanzania.

Amefafanua miongozo hiyo akisema iliangazia  “ni namna gani tunaweza kuhakikisha watalii wanakuwa salama na sisi wenyeji tuko salama. Kama unavyofahamu Wizara ya Afya na Wizara ya utalii tumekuwa tunashirkiana kwa karibu kuhakikisha tunaandaa miongozo kuhakikisha taratibu zinaweza kutumika kuona wageni na wenyeji wako salama. Mfano kuhakikisha watu wote wanavaa barakoa, wananawa  mikono, wanaweka umbali kati ya mtu mmoja na mwingine, lakini pia kupunguza mikusanyiko isiyo ya lazima. “ 

Mkurugenzi Mwendeshaji huyo wa TTB akaenda mbali kuzungumzia kile kilichoendelea baada ya kuandaa mwongozo akisema kuwa, “baada ya Baraza hilo kupata mwongozo tulioandaa na pia kutuma watu kuja kujihakikishia kuwa Tanzania iko salama, basi  waliitunuku Tanzania mhuri huo. Mhuri huo utasaidia sana kuwapatia tumaini na pia kuhakikishia watalii waliopata kuja Tanzania hasa wakati huu wa kipindi cha COVID-19 kwamba kwamba watakapokuja watakuwa salama na watarejea wakiwa salama.” 

Akizungumzia tamko la kisera la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuhusu athari za COVID-19 kwenye utalii duniani na hatua za kuchukua, Bi. Mdachi amesema, “ni kweli kuwa Tanzania haikuwa na idadi kubwa ya visa vya Corona lakini kwa kiasi fulani biashara ziliathirika mfano wa utalii, kampuni nyingi za kitalii zilishindwa kufanya kazi. Kama unavyofahamu utalii wa Tanzania unategemea  zaidi utalii wa kimataifa kuliko utalii wa ndani. Na kutokana na utalii wa kimataifa ambao tumekuwa tunapata mapato mengi, kwa hiyo kuwepo kwa wagonjwa wengi kwenye nchi ambazo tunapata watalii wengi kuja Tanzania, ilifanya sekta ya utalii Tanzania kuyumba. Nchi hizo zilizuia raia wao kusafiri nje ya mipaka, na pia mashirika mengi ya ndege yaliyokuwa yanaleta watalii,  yalisitisha huduma zao kuja Tanzania.” 

Devotha Mdachi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, TTB, wakati wa mahojiano na UNIC Dar es salaam.
UN/Ahimidiwe Olotu
Devotha Mdachi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, TTB, wakati wa mahojiano na UNIC Dar es salaam.

Hata hivyo ametoa shukrani akisema “tunashukuru kuwa Rais wetu kwa kutambua umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, hakufunga mipaka, lakini kupitia Wizara ya Afya wanaweka miongozo mbalimbali na wanatumia vyombo vya habari kuhakikisha watanzania wanaelewa jinsiya kukabilianana ugonjwa huo na matokeo tunaona idadi ya maambukizi  yalishuka na Rais aliruhusu biashara ziendelee na matokeo yake wageni kutoka nchi mbalimbali wameweza kuona na kuvutiwa na kuamini kuwa Tanzania ni salama. Kwa hiyo tumeona kuwa biashara zimeanza zimefunguka na mashirika ya ndege yameanza kurudi Tanzania na maisha yamerudi kama zamani.” 

Kuhusu hatua za kulinda wanyama walio hatarini kutoweka kama vile tembo, Mkurugenzi Mwendeshaji huyo amesema kuwa, Wizara ya Utalii imechukua hatua kudhibiti ujangili na uharamia ambapo imeanzisha jeshi usu kwani, “baadhi ya taasisi zake zina askari  ambao wamekuwa wakilinda na kutunza hifadhi zetu na tumeona matokeo yake. Mwaka 2014 katika hifadhi ya Mkomazi iliyoko mkoa wa Tanga na Kilimanjaro, idadi ya tembo ilipungua na kufikia 80 tu , lakini mwaka jana kwa muijbu wa takiwmu tulizo nazo idadi imeongezeka nakufikia 1,200. Hiki ni kiashiria tosha kuwa kuna hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara na taasisi zake kuhakikisha kuwa hifadhi inaendelea.”