Filamu ya Royal Tour Tanzania ni mkombozi wa sekta ya utalii 

Mtazamo wa maeneo ya forodhani visiwani Zanzibar.
UN News/Assumpta Massoi
Mtazamo wa maeneo ya forodhani visiwani Zanzibar.

Filamu ya Royal Tour Tanzania ni mkombozi wa sekta ya utalii 

Ukuaji wa Kiuchumi

Hatimaye filamu ya Tanzania The Royal tour iliyotengenezwa kuonesha vivutio vya utalii katika taifa hilo la Afrika Mashariki imezinduliwa nchini Marekani huku Msemaji Mkuu serikali ya Tanzania akisema filamu hiyo itakuwa mkombozi wakati huu ambapo mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania zinahaha kujikwamua kiuchumi baada ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. 

 

Soundcloud

Filamu hiyo ya dakika 56 inaonesha vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania Bara kama vile mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Taifa ya Serengenti, na kule Tanzania Zanzibar, hoteli za kitalii ikiwemo iliyoko ndani ya bahari huko Pemba,  huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kiongozi wa kutoa maelezo kuhusu vivutio hivyo kwa Peter Grenberg, ambaye ni mwanahabari nguli na mtozi wa filamu kutoka kituo cha televisheni cha CNBC nchini Marekani. 

Filamu inaenda kuleta mapinduzi kwenye utalii 

Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji Mkuu wa serikali ya Tanzania akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa baada ya uzinduzi uliofanyika jijini New York, Marekani mapema wiki hii amesema, “filamu hii ni mkombozi kwa nchi yetu kwa sababu unafahamu kwa muda mrefu tumekuwa tukihangaika kwa muda mrefu kutafuta majukwaa ya kimataifa ya namna gani ya kutangaza vivutio vya utalii. Tanzania imetajwa na tafiti mbalimbali kuwa ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya utalii.” 

Amesema ingawa ya kuwa na vivutio hivyo bado kuna changamoto ya watu kufahamu juu ya uwepo wa vivutio hivyo kwa hiyo kupitia waandaaji wa filamu hiyo, wataweza kutangaza filamu hiyo kwa hadhara kubwa zaidi ya kimataifa na hatimaye idadi ya watalii kuongezeka kutoka milioni 1.7 wa nje na wa ndani kwa mwaka hivi sasa hadi milioni 5.  

“Tumepiga hatua kubwa kutoka watalii 620,000 wakati COVID-19 ilipoingia na hii ilituathiri sana, lakini baada ya kuwa tumechukua hatua mbalimbali, tumezingatia taratibu za shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, sasa idadi ya watalii imeongezeka, watalii wengi wana imani kuwa wakija Tanzania wanakuwa salama,” amesema Bwana Msigwa. 

Amesema idadi inaongezeka na filamu itawapeleka kwenye ndoto ya taifa hilo ya kufikisha watalii milioni 5 kwa mwaka. 

Mji Mkongwe, Zanzibar, Tanzania.
Unsplash/Kaspars Eglitis
Mji Mkongwe, Zanzibar, Tanzania.

Matokeo ya ujio wa watalii ni manufaa kwa mwananchi 

Msemaji huyo amefafanua kuwa mapato kutokana na utalii yatachangia katika ujenzi wa miundombinu kama vile ya afya na ya kijamii zikiwemo shule, maji, barabara na vituo vya afya  bila kusahau mikopo kwa elimu ya  juu na kulipia gharama za elimu ya msingi na sekondari ambayo ni bure kwa kuwa serikali inalipa zaidi ya shilingi bilioni 26 kila mwezi kuhakikisha watoto wanapata elimu hiyo bila malipo. 

Kwa kufanya hivyo amesema, utalii utachangia katika ufanikishaji wa malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs yanayofikia ukomo mwaka 2030. 

Kuna miundombinu kuhakikisha utalii endelevu 

Wakati Umoja wa Mataifa unatilia mkazo utalii endelevu usioharibu mazingira, Bwana Msigwa amesema kile ambacho Umoja wa Mataifa kinaelekeza ndicho ambacho Tanzania inazingatia kupitia diplomasia majumui au Multilateral Diplomacy.  

“Tunazingatia maeneo ya  utalii hayaharibiwi, maeneo ya utalii yanakuwa rafiki kwa watalii, usalama kwa watalii unakuwepo na zaidi ya hapo, tunatunza mazingira kwa ajili ya utalii. Nchi yetu asilimia 32 ya eneo lake lote ni ni maeneo ya hifadhi,” amesema Bwana Msigwa. 

Ametaja mradi wa REGROW unaotekelezwa kusini mwa Tanzania kupitia fedha kutoka Benki ya Dunia akisema, “tunaenda kutumia shilingi bilioni 350 sawa na zaidi ya dola milioni 150, kuhakikisha tunaweka miundombinu, usalama na kutunza mazingira, ili mazingira yawe rafiki kwa utalii. Na hayo tunapata kupitia diplomasia majumui.” 

Umoja wa Mataifa una mchango mkubwa kwa Tanzania 

Bwana Msigwa amesema miradi lukuki inatekelezwa Tanzania kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa kwenye afya, elimu na miundombinu kupitia mashirika kama vile WHO, FAO, UNICEF na IFAD akisema “Rais ameelekeza kuwa sasa tunashirikiana pamoja na Umoja wa Mataifa na tunashiriki kikamilifu.”