Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumuenzi Malkia Elizabeth kwa kufanya kazi kwa bidii ili tuwe UN ya kweli- Katibu Mkuu

Mwaka 2010, Malkia wa Elizabeth wa II wa Uingereza akiweka shada la maua kwenye eneo la kukumbuka watumishi wa UN waliopoteza maisha yao wakihudumia shirika.
UN /Evan Schneider
Mwaka 2010, Malkia wa Elizabeth wa II wa Uingereza akiweka shada la maua kwenye eneo la kukumbuka watumishi wa UN waliopoteza maisha yao wakihudumia shirika.

Tumuenzi Malkia Elizabeth kwa kufanya kazi kwa bidii ili tuwe UN ya kweli- Katibu Mkuu

Masuala ya UM

Jua limezama kwa mtawala wa aina yake! Ndivyo alivyoanza hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo kwenye ukumbi wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani, ambamo wawakilishi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa walikutana katika tukio maalum la kuenzi Malkia Elizabeth wa II wa Uingereza aliyega dunia tarehe 8 mwezi huu wa Septemba huko Scotland.

Katibu Mkuu ametumia hotuba yake hiyo ya kurasa mbili kumwelezea Hayati Malkia Elizabeth aliyeongoza Uingereza, Ireland Kaskazini, Scotland na Wales pamoja na mataifa mengine yaliyokuwa chini ya himaya ya Uingereza.

Alikuwa mhimili bila ya kuwa mwinyi

“Kwa zaidi ya miaka 70, alikuwa mhimili bila kuwa mwinyi kwenye jukwaa la dunia akishika uongozi kwenye zama za Churchill, Truman, Stalin, Maon na De Gaulle,” akimaanisha viongozi wa Uingereza, Marekani, Urusi, China na Ufaransa, ambazo ni nchi zenye ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Amesema Malkia Elizabeth wa II ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96, katika kipindi chote cha uhai wake, alikuwa nanga ya utulivu hata wakati hali ilipotibuka.

Guterres amesema wakati wa uongozi wake, ilishuhudiwa mataifa mengi yakipata uhuru kutoka Uingereza na kuanzishwa kwa Jumuiya ya Commonwealth, kundi la ushirikiano wa kimataifa lenye wanachama tofauti tofauti.

Amezungumzia pia kitendo cha Malkia Elizabeth wa II alipotembelea Afrika Kusini na kuzungumzia ni kwa vipi imani inaweza kuhamisha milima na kujenga upya mataifa. Wakati huo Afrika Kusini ilijiunga tena na Jumuiya ya Commonwealth baada ya kuporomoka kwa ubaguzi wa rangi.

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia, serikali ya Uingereza na Jumuiya ya Commonwealth akielezea pia jinsi Malkia huyo alikinzana na nguvu za kisiasa na kijiografia.

Aliunga harakati za ushirikiano wa kimataifa

Katibu Mkuu ameendelea kumwelezeaa akisema, “Alikuwa mwanadiplomasia wa kipekee. Mara nyingi alitumia stadi zake za kidiplomasia kama mwanamke pekee ndani ya chumba. Wakati taasisi yetu ilikuwa changa kama alivyokuwa yeye mwenyewe wakati huo, alisimama kwenye mimbari hii hii na kutoa wito kwa viongozi kuonesha kujitolea kwao kwa maadili ya Chata ya Umoja wa Mataifa.”

Katika maelfu ya matukio yake kwa umma ,Malkia Elizabeth alizungumzia urafiki na ushirikiano thabiti baina ya mataifa. “Aliunga mkono harakati lukuki za kimataifa ambazo zilikuwa ndani ya moyo wake.”

Amerejelea hotuba yake kwenye ukumbi wa Baraza Kuu miaka 12 iliyopita ambapo alisema katika kipindi cha maisha yake, “Umoja wa Mataifa umekua kutoka chombo chenye matamanio makubwa hadi kuwa shinikizo thabiti la maslahi ya wengi. Katika dunia yake kesho lazima tushirikiane kuliko wakati wowote ule iwapo tunataka kweli kuwa Umoja wa Mataifa.”

Ni kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu ameisihi jamii ya kimataifa kumuenzi Malkia Elizabeth kwa kufanya kazi kuliko wakati wowote ule ili kuwa Umoja wa Mataifa wa kweli.

Kőrösi arejelea kauli ya Malkia Elizabeth kuhusu uongozi na mwelekeo wa UN

Naye Rais wa Baraza Kuu la UN, Csaba Kőrösi, ametumia hotuba yake kukumbuka jinsi Malkia Elizabeth alivyotembelea UN mwaka 2010 na kuvutiwa na wale wenye kipaji cha kuongoza, hasa kwenye huduma ya umma na kidiplomasia.

Amemnukuu aliposema, “baadhi ya sifa za viongozi, ni za kimataifa, na mara nyingi zinapata fursa ya kuhamasisha watu na kuunganisha juhudi zao, vipaji vyao, mitazamo yao na matamanio yao ili kufanya kazi Pamoja.”

Bwana Kőrösi amesema, “pindi Umoja wa Mataifa utakapofanyiwa tathmini na vizazi vijavyo, matumai ya Malkia Elizabeth ni kwamba itakuwa uaminifu wetu, utayari wetu wa kuongoza na azma yetu ya kufanya kile kilicho sahihi, hivyo vitafaulu mtihani wa nyakati.”

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema, “mfannao kati ya maneno yake na maelezo ya sifa zake viko dhahiri. Alijitolea uhai wake kwenye huduma kwa umma na kuboresha maisha ya watu ndani ya Jumuiya ya Commonwealth.”