Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Buriani Malkia Elizabeth II - Katibu Mkuu UN

Malkia Elizabeth II wa Uingereza alipohutubia Baraza Kuu
UN Photo
Malkia Elizabeth II wa Uingereza alipohutubia Baraza Kuu

Buriani Malkia Elizabeth II - Katibu Mkuu UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa sana na kifo cha Malkia Elizabeth II, ambaye ni Malkia wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini .

Kupitia taarifa iliyotolewa na na msemajiwake mchana huu kwenye Umoja wa Mataifa New York Marekani , Antonio Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Malkia, serikali na watu wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini na pia nchini zote za jumuiya ya Madola.

Akiwa Mkuu wa nchi aliyeishi muda mrefu zaidi na aliyetawala muda mrefu zaidi nchini Uingereza, Malkia Elizabeth II alisifiwa sana kwa wema wake, utu na kujitolea kwake kote ulimwenguni. 

Malkia Elizabeth wa pili ambaye ameaga dunia leo akiwa na umri wa miaka 96 akikuwepo kutia moyo moyo katika miongo yote ya mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kukomeshwa kwa ukoloni Afrika na Asia na mageuzi ya Jumuiya ya Madola.

Guterres amesema “Malkia Elizabeth II alikuwa rafiki mkubwa wa Umoja wa Mataifa, na alitembelea Makao Makuu yetu ya New York mara mbili, zaidi ya miaka hamsini tofauti. Alijitolea sana kwa sababu nyingi za usaidizi na mazingira na alizungumza kwa hisia kwa wajumbe katika mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow.”

Malkia Elizabeth II
UN
Malkia Elizabeth II

Katibu Mkuu ametoa pongezi kwa Malkia Elizabeth II kwa kujitolea kwake bila kuyumbayumba katika kuwatumikia watu wake. 

Akiongeza kuwa ulimwengu utakumbuka kwa muda mrefu kwa sababu ya kujitolea na uongozi wake.

Kwa mujibu wa duru za habari Malkia Elizabeth alitawazwa kuwa malkia mwaka 1952 na amekuwa madarakani kwa miongo 70 kabla y amauti kumfika. 

Malkia Elizabeth ndiye malkia aliyetawala kwa muda mrefu zaidi nchini Uingereza. 

Na kwa mujibu wa sheria za Uingereza mara baada ya kufaridi dunia malkia mrithi wake ambaye ni Prince Charles anashika hatamu mara moja hivyo kuannzia sasa amekuwa Mfalme Charles III.

Watoto wakimkabidhi maua Malkia Elizabeth II wa Uingereza wakati akihitimisha ziara yake kwenye Umoja wa Mataifa New York Marekani
UN Photo/Mark Garten
Watoto wakimkabidhi maua Malkia Elizabeth II wa Uingereza wakati akihitimisha ziara yake kwenye Umoja wa Mataifa New York Marekani

Siku za mwisho huko Scotland

Malkia Elizabeth II amekufa kwenye inayojulikana kama Ngome ya Balmoral huko Scotland, ambayo ilikuwa kama makazi ya kifalme ya majira ya joto.
Katika mwaka uliopita, Malkia alikuwa amekabidhi majukumu ya kifalme kwa mtoto wake mkubwa, mwanamfalme Charles au Prince Charles, mrithi wa kiti cha enzi, pamoja na kusimamia ufunguzi wa bunge  hapo mwezi Mei mwaka huu. Na hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 1963 Malkia hakuweza kuhudhuria sherehe hiyo.
Malkia alipita wakati wa hali tete kisiasa baada ya maziri mkuu Boris Johnson kujiuzulu hivi karibuni. Waziri Mkuu Mpya Liz Truss alisafiri Jumanne hadi kwenye kasri la kifalme huko Scotland, ili kupewa jukumu rasmi la kuunda serikali.
Bi Truss amekua waziri mkuu wa 15 kushika wadhifa huo wakati wa utawala wa malkia  na Waziri mkuu wa kwanza wa utawala wake alikuwa Winston Churchill.

Malkia Elizabeth II wa Uingereza akihutubia Baraza Kuu la UN Oktoba 1957
UN Photo/Albert Fox
Malkia Elizabeth II wa Uingereza akihutubia Baraza Kuu la UN Oktoba 1957


Maisha ya malkia

Malkia Elizabeth II alitawazwa kukalia kiti cha enzi baada ya kifo cha babake Mfalme George VI tarehe 6 Februari 1952, akiwa na umri wa miaka 25 tu na mwezi Juni mwaka uliofuata alitawazwa rasmi kuwa malkia wa Uingereza na Ireland ya Kaskazini.
Mwezi Februari mwaka huu, Uingereza ilianza mfululizo wa sherehe za Jubilee ya Platinum ya Malkia, kuadhimisha miaka 70 ya utawala wake kwa Jumuiya ya Madola ya Uingereza.
Katika kipindi chote cha uongozi wake, Malkia Elizabeth II alihudumu kama kiungo hai cha wakati wa vita ya pili ya dunia kwa taifa lake la Uingereza na aliongoza marekebisho ya enzi ya baada ya ukoloni na alilishuhudia taifa lake likipitia kile ambacho wengine walikiita "talaka kali" kutoka kwa Muungano wa Ulaya wakati wa Brexit.

Malkia Elizabeth II akitia saini kitabu cha wageni kwenye makao makuu ya UN New York
UN Photo/Mark Garten
Malkia Elizabeth II akitia saini kitabu cha wageni kwenye makao makuu ya UN New York

Kwaheri Malkia Elizabeth II

Baada ya kutangazwa kwa kifo chake, umati wa watu ulianza kumiminika nje ya kasri la la kifalme la Buckingham  na unaendelea kuongezeka huku wengine wakistahimili kunyesha kwa mvua kubwa huko Balmoral Scotland aliokofia kwenye kasri la familia yake 
Tovuti rasmi ya familia ya kifalme haikupatikana muda mfupi baada ya kifo chake lakini ilichapisha kwamba Malkia alikufa kwa amani.
Iliongeza kuwa mtoto wake Charles na mkewe Camilla, Mfalme na Malkia Consort, "watasalia Balmoral jioni hii na watarejea London kesho".
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, kutakuwa na kipindi cha siku 10 kabla ya mazishi yake kufanyika.