Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Prince Phillip afariki dunia, Guterres atuma rambirambi

Prince Phillip ambaye ni Duke of Edinburgh (kushoto) alipokutana na hayati Kofi Annan, Katibu Mkuu wa UN huko Edinburgh, Scotland mwaka 2005.
UN Photo/Evan Schneider
Prince Phillip ambaye ni Duke of Edinburgh (kushoto) alipokutana na hayati Kofi Annan, Katibu Mkuu wa UN huko Edinburgh, Scotland mwaka 2005.

Prince Phillip afariki dunia, Guterres atuma rambirambi

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea masikitiko yake kufuatia kifo cha mume wa Malkia wa Uingereza, Prince Phillip ambaye amefariki dunia leo. Alikuwa na umri wa miaka 99.

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Bwana Guterres akituma salamu zake za rambirambi kwa Malkia Elizabeth wa II, na watu wa Uingereza.

Guterres amesema Prince Phillip ambaye ni Duke wa Edinburgh, kwa uwezo wake wote alimsaidia Malkia katika majukumu yake ya uongozi wa Uingereza kwa miaka 60.

Tweet URL

“Alitambuliwa kwa kujitoa kwake kwa dhati katika masuala ya kujitolea akiwa mlezi wa zaidi ya mashirika 800, hususan yale yaliyojikita katika masuala ya mazingira, viwanda, michezo na elimu,” amesema Guterres.

Halikadhalika mchango wake katika ustawi bora wa wakazi wa dunia.

Prince Phillip amefariki dunia leo asubuhi kwa saa za Uingereza kwenye kasri ya Windsor na alikuwa na umri wa miaka 99.

Viongozi mbalimbali watuma salamu za rambirambi

Kufuatia kifo cha Prince Phillip, viongozi mbalimbali wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wametumia mtandao wa Twitter kutuma salamu za rambirambi  na miongoni mwao ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, Dkt. Tedros Ghebreyesus.

Katika ujumbe wake amesema, “nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Prince Phillip, Duke wa Edinburgh na natuma salamu za rambirambi kwa mkewe Malkia Elizabeth, familia ya kifalme na wananchi wa Uingereza.”

Naye Ngozi Okonjo-Iweala, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la biashara duniani, WTO amesema, “nimesikitishwa na kifo na natuma salamu za rambirambi kwa Malkia Elizabeth wa II, Waziri Mkuu Boris Johnson na zaidi kwa Prince William.”

David Milpass, Mkurugenzi Mkuu wa Benki  ya Dunia amemwelezea Prince Phillip kama mtu ambaye alikuwa amejitolea kwa huduma za umma na kuwa na uchanya katika maisha. Ametuma salamu za rambirambi kwa Malkia Elizabeth wa II, familia ya kifalme na serikali na wananchi wa Uingereza huku akisema yuko pamoja nao wakati  huu wa kipindi cha majonzi.