Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tubadili mtazamo kwamba Afrika ni bara tegemezi:Amina Mohammed 

Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed (Desemba 2019)
UN Video
Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed (Desemba 2019)

Tubadili mtazamo kwamba Afrika ni bara tegemezi:Amina Mohammed 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Bara la Afrika ni tajiri sio tu kwa maliasili yake, lakini pia kwa idadi yake ya vijana wenye nguvu.  

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kubadili sura ya Afrika na mtazamo kwamba  bara hilo ni tegemezi na kuzisaidia nchi za eneo hilo katika maendeleo ya mifumo ya kisasa ya nishati na chakula. 

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, wakati akizungumza nchini Tunisia kwenye Mkutano wa nane wa kimataifa wa Tokyo ambao ni wa siku mbili kuhusu maendeleo ya Afrika. 

Amina Mohamed amesisitiza kuwa, nchi za Afrika zina viashiria vyote vinavyohitajika kwa maendeleo endelevu, na ushirikiano wao katika uchumi wa dunia utafanya uwezekano wa kuondokana na vikwazo vingi vya sasa.  

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa anaamini kuwa jumuiya ya kimataifa inadharau uwezo wa bara hilo. 

Bara changa 

 Zaidi ya watu bilioni 1.2 wanaishi barani Afrika. Takriban asilimia 60 ya wakazi wa Afrika wana umri wa chini ya miaka 35.  

Ukuaji wa haraka wa miji katika nchi za Afrika unaahidi fursa mpya, ikiwa ni pamoja na katika uwanja wa maendeleo ya viwanda kwenye bara hilo. 

Amina Mohammed ametaja hati mbili kama ramani ya barabara kwa maendeleo endelevu ya bara hilo ambazo ni malengo ya maendeleo endelevu na ajenda ya 2063 ya Afrika. 

Matokeo ya Kuporomoka 

Bi. Mohammed amesisitiza kuwa ili kufanikiwa kufikia malengo ya ajenda hizi mbili jumuiya ya kimataifa lazima ishirikiane kuondoa athari za migogoro mingi. 

"Kujikwamua kutoka kwa janga la COVID-19, matokeo ya vita nchini Ukraine, dharura ya hali ya mabnadiliko ya tabianchi na shida ya kifedha inaweka idadi ya watu walio hatarini zaidi kwenye mtihani.”  

Ameongeza kuwa mchanganyiko huo unaolipuka hutengeneza mazingira yenye rutuba ya kuzidisha migogoro iliyopo na ya siku zijazo na huzaa machafuko, ambayo yanadhoofisha juhudi za pamoja za kufikia malengo ya SDGs. 

Amina Mohammed amekumbusha kuwa eneo la biashara huria la Afrika, linachangia ukuaji wa viwanda, mchanganyiko na uchumi wa kidijitali wa nchi za kanda hiyo, na pia husaidia kuimarisha ushirikiano wa kikanda. 

Mikakati mitatu ya hatua 

Naibu Katibu Mkuu ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanyia kazi mambo matatu ambayo yatanufaisha uchumi wa Afrika na kusaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu. 

Kwanza, kama alivyosema, ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa vyanzo vya nishati kwa wote na mabadiliko ya haki na ya usawa kwa vyanzo vya nishati mbadala.  

Katika muktadha huu, Bi. Amina Mohammed ametoa wito wa kuwepo kwa mbinu jumuishi ili kuongoza maendeleo ya nishati barani Afrika, kwa kuzingatia uwekezaji endelevu na ushirikiano imara. 

Amesema “Leo, takriban watu milioni 600 barani Afrika wanakabiliwa na uhaba wa umeme. Na hii ina maana kwamba bara litahitaji taratibu za maendeleo ya vyanzo vya nishati rafiki kwa mazingira. Kupanda kwa sasa kwa bei ya nishati kunaweza pia kuhimiza nchi za Afrika kutumia vyema uwezo mkubwa wa nishati mbadala wa bara hilo. Lakini hii inahitaji uwekezaji mkubwa na wa wakati.” 

 Pili, Afrika inahitaji mabadiliko ya haraka ya mifumo yake ya chakula. 

"Ili Afrika iwe kikapu halisi cha mkate, ni muhimu kufikia ongezeko la uzalishaji katika kilimo na mifumo ya chakula, kutumia teknolojia mpya na mifumo ya kisasa ya umwagiliaji, kufikia kilimo cha ufundi na kupunguza hasara baada ya mavuno...", amesisitiza mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa. 

 Hatimaye tatu, matatizo ya Afrika, yanayosababishwa na migogoro inayoingiliana, hayatatatuliwa bila kushughulikia ukosefu wa usawa, anesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa. 

"Ni muhimu kubadili mtazamo wa Afrika kama bara tegemezi, na kuifanya kuwa mhusika mkuu katika hatua ya dunia, yenye haki na nafasi sawa, iwe ya kiuchumi au kisiasa, kama ukanda mwingine wowote," amehitimisha Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.