Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukeketaji Sierra Leone ni ukatili wa kupitiliza unaopaswa kukomeshwa:UN

Mwanamke akiwa ameshikilia kisu kilichotumika kwenye ukeketaji.
UNICEF/Catherine Ntabadde
Mwanamke akiwa ameshikilia kisu kilichotumika kwenye ukeketaji.

Ukeketaji Sierra Leone ni ukatili wa kupitiliza unaopaswa kukomeshwa:UN

Haki za binadamu

Wataalamu huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa leo wametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi za kuzuia na kuadhibu vitendo vya ukeketaji wa wanawake nchini Sierra Leone.

Kufuatia kesi ya jinai juu ya kifo cha mwanafunzi mwenye umri wa miaka 21 aliyefanyiwa vitendo hivyo vya kikatili katika wilaya ya Bonthe, nchini humo wataalam hao maalum watatu wametoa tamko la kulaani ukeketaji wakiuita kuwa ni "aina mbaya zaidi ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ambayo ni sawa na mateso”. 

Wameongeza kuwa ukeketaji "Unakiuka haki za msingi za waathriwa wake, ikiwa ni pamoja na hadhi yao ya kimwili na haki za kutoteswa au kutendewa vitendo vingine vya kikatili na haki ya maisha, afya ya ngono na uzazi.” 

Mazoezi yaliyokita mizizi  

Wataalam hao katika taarifa yao wamesema ukeketaji ni desturi za kibaguzi na  zimejikita katika kanuni za kijamii na uchu wa mamlaka, bila shaka unaohusishwa na hadhi na nafasi ya mtu katika jamii. 

"Kama desturi zingine za asili zenye madhara za asili kama hiyo, ukeketaji unaonyesha na kuendeleza mwelekeo mpana wa ukosefu wa usawa wa kijinsia". 

Watatu hao wamesisitiza kuwa ukeketaji hauwezi kurekebishwa au kutumiwa kama uhalali wa kutumia mila za kitamaduni na kidini kwa kuhatarisha ustawi wa wanawake na wasichana. 

Wameongeza kuwa ni "Lazima mila hizo zifafanuliwe kulingana na mwelekeo mpana wa unyanyasaji wa kijinsia, ambao hauwezi kuendelea bila kuadhibiwa.”  

Ngariba na mjukuu wake wa miaka 10 ambaye alikuwa anatarajiwa kukeketwa lakini anaumwa kwa hiyo bibi yake anasubiri naye.
UNFPA/Georgina Goodwin
Ngariba na mjukuu wake wa miaka 10 ambaye alikuwa anatarajiwa kukeketwa lakini anaumwa kwa hiyo bibi yake anasubiri naye.

Haki ya mahakama inahitajika 

Kwa mujibu wa ripoti, kesi ya jinai dhidi ya mmoja wa wahalifu wanaoshtakiwa kwa ukeketaji uliosababisha kifo cha mwathiriwa imezuiliwa na kushindwa kuwepo kwa utaratibu wa kuwalinda wanawake na wasichana. 

"Kukosekana kwa sheria inayojitolea na inayotekelezeka ambayo inaharamisha na kuadhibu kwa uwazi ukeketaji kunazuia uchunguzi wa mahakama au uchunguzi mwingine kuhusu watu kuteswa na vitendo hivi hatari na mauaji haramu," wamesema wataalam hao. 

Wameongeza kuwa "Sheria na sera zinahitaji kutoa mifumo ya wazi ya uwajibikaji na vikwazo vya kinidhamu kuhusiana na ukeketaji.” 

Kusaidia wanawake 

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameitaka Serikali ya Sierra Leone kuanzisha vifungu maalum vya kisheria vinavyokataza vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha mkataba wa maelewano na watendaji wa ndani na kurekebisha sheria ya haki za mtoto ili kupiga marufuku kwa uwazi ufanyaji wa tohara kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 18. 

Wakati huo huo, wamekaribisha tangazo la Rais wan chi hiyo la nia yake ya kuunga mkono mswada wa uzazi usio na hatari, ambao utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ya ngono na uzazi kwa wanawake na wasichana. 

"Sierra Leone inachukua hatua madhubuti na za maana katika kuendeleza haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na hatua ya hivi karibuni ya kukomesha adhabu ya kifo," wamehitimisha taarifa yao wataalam hao.