Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka Hiroshima, Mkuu wa UN: Njia pekee ya kukabiliana na tishio la nyuklia ni kutokuwa na silaha za nyuklia

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia katika sherehe ya Kumbukumbu ya Amani huko Hiroshima, Japan.
UN Photo/Ichiro Mae
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia katika sherehe ya Kumbukumbu ya Amani huko Hiroshima, Japan.

Kutoka Hiroshima, Mkuu wa UN: Njia pekee ya kukabiliana na tishio la nyuklia ni kutokuwa na silaha za nyuklia

Amani na Usalama

Ni jambo lisilokubalika kabisa kwa mataifa yenye silaha za nyuklia kukiri uwezekano wa vita vya nyuklia, Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Maataifa Antonio Guterres, Jumamosi nchini Japan katika sherehe za kuadhimisha miaka 77 ya shambulio la bomu la nyuklia la Hiroshima.

“Silaha za nyuklia ni upuuzi. Ikiwa imeshapita robo tatu ya karne, lazima tujiulize tumejifunza nini kutokana na wingu la uyoga ambalo lilitanda juu ya jiji hili mnamo mwaka 194”, amesisitiza wakati wa hafla hiyo kwenye Hifadhi ya kumbukumbu ya Amani ya Hiroshima iliyohudhuriwa na watu kadhaa, akiwemo Hibakusha- wanaharakati wa amani vijana , Waziri Mkuu wa Japan na viongozi wengine katika ngazi ya kijamii.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya kwamba, mbio mpya za silaha zinashika kasi na viongozi wa dunia wanaongeza hifadhi kwa gharama ya mamia ya mabilioni ya dola na takriban silaha za nyuklia 13,000 zimehifadhiwa kwa sasa katika maghala duniani kote.

“...Migogoro yenye sauti kubwa ya chini ya nyuklia inaenea kwa kasi kutoka Mashariki ya Kati hadi rasi ya Korea, hadi uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ... Ubinadamu unacheza na bunduki iliyojaa”, alionya.

Tweet URL

Ishara za matumaini

Katibu Mkuu Guterres aliutaja Mkutano wa sasa wa Mapitio ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia huko New York kuwa ni ‘ishara ya matumaini’.

“Leo, kutoka katika sehemu hii takatifu, natoa wito kwa wanachama wa Mkataba huu kufanya kazi kwa haraka ili kuondoa akiba ambayo inatishia maisha yetu ya baadaye, kuimarisha mazungumzo, diplomasia na mazungumzo, na kuunga mkono ajenda yangu ya upokonyaji silaha kwa kuondoa vifaa hivi vya uharibifu”, alisisitiza.

Ameongeza kuwa nchi zilizo na silaha za nyuklia lazima zijitolee “kutozitumia mara ya kwanza” na kuwahakikishia mataifa mengine kwamba hazitatumia au kutishia kutumia silaha za nyuklia dhidi yao.

“Lazima tuzingatie hofu za Hiroshima kila wakati, kwa kutambua kuna suluhisho moja tu la tishio la nyuklia: kutokuwa na silaha za nyuklia hata kidogo”, mkuu wa UN alisema.

Mabaki ya jengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki. Majengo yalisalia magofu.
UN /DB
Mabaki ya jengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki. Majengo yalisalia magofu.

Wakati wa kueneza amani

Guterres alisisitiza kuwa viongozi hawawezi kujificha kutotimiza majukumu yao.

“Ondoa chaguo la nyuklia kwenye meza kwa manufaa. Ni wakati wa kueneza amani. Sikiliza ujumbe wa hibakusha: “Hakuna Hiroshimas tena! Hakuna Nagasakis tena!”, alisema.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alihitimisha hotuba yake kwa kutuma ujumbe kwa vijana hao akiwataka wamalize kazi ambayo hibakusha imeanza.

“Ulimwengu haupaswi kusahau yaliyotokea hapa. Kumbukumbu ya wale waliokufa na urithi wa wale walionusurika haitazimika kamwe”. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atakuwa nchini Japan mpaka mwishoni mwa juma, ambapo atakutana na maafisa kadhaa wakuu wa Japan, akiwemo Waziri Mkuu Fumio Kishida.

Pia atakutana na kundi la wahanga walionusurika wa mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki, na kushiriki katika mazungumzo na wanaharakati vijana ambao wanaongoza mipango juu ya upunguzaji wa silaha za nyuklia, kutoeneza na maswala mengine ya kimataifa.