Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajabu miaka 73 baada ya Hiroshima bado nyuklia zashamiri- Guterres

Saa ya mkononi ilivyosalia baada ya bomu la Hiroshima. Saa hii inaonyesha ilisimama saa 2.15 asubuhi punde tu baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki tarehe 6 Agosti 1945.
UN /Yuichiro Sasaki

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mnepo wa mji wa Hiroshima nchini Japan na wakazi wake baada ya kupigwa na bomu la atomiki miaka 73 iliyopita ni jambo la kupongezwa kwa kuzingatia madhila waliyopitia.

Bwana Guterres amesema hayo katika hotuba iliyosomwa hii leo huko Hiroshima kwa niaba yake na Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa  Mataifa kuhusu masuala ya kuondokana na silaha, Izumi Nakamitsu.

Amezungumzia Hibakusha ambao ni manusura wa shambulio la wakati huo na waliozaliwa na athari za bomu hilo, akisema ni majasiri kutokana na kuendeleza harakati za maridhiano na amani.

Bwana Guterres amesema licha ya athari za silaha za nyuklia kuwa dhahiri, ni ajabu kuwa bado kasi ya kutengeneza silaha za nyuklia inaongezeka.

 Miaka 73 baada ya bomu la atomiki kuangushwa huko Hiroshima nchini Japan, bado baadhi ya mataifa yanaendelea na kasi ya kusongesha silaha hizo.

Mabaki ya moja ya majengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki Agosti 6, 2018
UN
Mabaki ya moja ya majengo huko Hiroshima nchini Japan baada ya kuangushwa kwa bomu la atomiki Agosti 6, 2018

“Mvutano baina ya mataifa yenye silaha za nyuklia unaongezeka. Silaha hizo zinazidi kutengenezwa kwa ubora zaidi na katika maeneo mengine zinaongezwa idadi,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa dunia inahitaji uongozi wa kimaadili wa Hibakusha na wakazi wa Hiroshima kwa jinsi wanavyoendelea kuelimisha umma juu ya madhara ya silaha za  nyuklia na tishio lake kwa usalama wa dunia na kibinadamu.

Amesema kiilichotokea Hiroshima tarehe 6 Agosti mwaka 1945 hakipaswi kutokea tena.

Kilichotokea Hiroshima hakipaswi kutokea tena

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amerejelea hatua ya mwaka jana ya kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa kuzuia silaha za  nyuklia akisema ni dhihirisho la kuungwa mkono suala la kuondokana na silaha hizo.

“Viongozi wa dunia wanapaswa kurejea kwenye mazungumzo na diplomasia na kuwa na mwelekeo mmoja wa kuondokana kabisa na silaha za nyuklia na  hatimaye kuwa na dunia salama zaidi kwa kila mtu,” amesema Katibu Mkuu.

Majeruhi baada ya kukimbia moto uliotokana na bomu la atomiki lililoangushwa saa 2.15 asubuhi, walikusanyika kwenye kingo ya barabara magharibi mwa Miyuki-bashi mjini Hiroshima saa tano asubuhi ya tarehe hiyo hiyo ya shambulio 6 Agosti 1945.
UN /Yoshito Matsushige

Amesema ni kwa kuzingatia hilo ndio maana mwezi Mei mwaka huu alizindua ajenda yake ya kuwa na mustakhbali wa pamoja kuhusu suala la kutokomeza kuenea kwa silaha.

Ametanabaisha kuwa ajenda hiyo hailengi kubadili wajibu wa serikali wa kuondokana na silaha hizo,  bali kuimarisha juhudi za pamoja kwa ajili ya amani na usalama duniani.

Katibu Mkuu  amesihi katika kumbukizi ya wahanga wa shambulio la Hiroshima hii leo, anarejelea azma yake ya kushirikiana na Hibakusha, wakazi wa Hiroshima na watu wote duniani ili kutimiza lengo la kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia.

Tarehe 6 Agosti mwaka 1945 Marekani iliangusha bomu la atomiki lenye uzito wa tani 5 kwenye mji wa Hiroshima na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.