Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana chonde chonde tunawategemea katika dunia isiyo na nyuklia- Guterres

Mji wa Nagasaki ulivyobaki baada ya kudondoshwa bomu la Atomiki, hapo ni umbali wa mita 700 kutoka kitovu cha mlipuko, kama ulivyoonekana  tarehe 10 Agosti 1945.
UN Photo/Yosuke Yamahata
Mji wa Nagasaki ulivyobaki baada ya kudondoshwa bomu la Atomiki, hapo ni umbali wa mita 700 kutoka kitovu cha mlipuko, kama ulivyoonekana tarehe 10 Agosti 1945.

Vijana chonde chonde tunawategemea katika dunia isiyo na nyuklia- Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema vitisho vya nyuklia bado vipo wakati huu ambapo kuna ongezeko la mvutano baina ya nchi zenye silaha hizo sambamba na kuyoyoma kwa mikataba ya kudhibiti silaha za nyuklia.

Bwana Guterres amesema hayo katika ujumbe wake aliotoa huko Nagasaki nchini Japan hii leo ikiwa ni miaka 74 ya kumbukizi ya kuangukwa kwa bomu la atomiki na Marekani kwenye mji huo tarehe 9 Agosti mwaka 1945.

Katika ujumbe huo uliosomwa kwa niaba yake na msaidizi wake wa masuala ya kudhibiti kuenea kwa silaha duniani, Izumi Nakamitsu, Katibu Mkuu amepongeza manusura wa shambulio hilo akisema ni kwa ujasiri wao, “Nagasaki iliibuka na kuwa nguzo ya amani na uelewa duniani.”

Katibu Mkuu amesema, “niliguswa mno pindi nilipofika mji wa Nagasaki mwaka jana kwa tukio kama la leo. Shuhuda za manusura au hibakusha ambao ni manusura jasiri, ziligusa moyo wangu sambamba na kujitolea kwao kuhakikisha kuwa janga hili katu halitakumba tena mji huu au mji mwingine.”

Amerejea pia hotuba yake ya mwaka jana ya hofu ya kuanza tena kwa tisho la nyuklia akisema kuwa, “jamii ya kimataifa lazima iungane kulinda manufaa ya kiusalama yanayoletwa na mikataba iliyopo. Lazima tufanye kazi pamoja tuimarishe ushirikiano, kuaminiana, uwazi ambavyo vyote ni msingi wa mazungumzo ya dhati na mashauriano.”

Bwana Guterres ametaka lakini hatua zaidi akisema kuwa. “hakikisho la kweli la kutokuwepo kwa silaha za nyuklia ni kutokomeza kabisa silaha hizo. Haya ndio matamanio yangu ya Umoja wa Mataifa na tunayapatia kipaumbele cha juu.”

Amesisitiza kuwa hakuna ushahidi mwingine thabiti wa kutosha zaidi ya shuhuda za hibakusha akisema kuwa, “nashukuru majiji ya Nagasaki na Hiroshima pamoja na serikali ya Japan kwa kutunza ushahidi huo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.”

Amewageukia vijana akisema kuwa, “kwenu ninyi vijana, wajenzi wa amani wa siku zijazo duniani, ujumbe wangu kwenu uko Dhahiri; ninyi ndio nguvu ya kutunza mustakabali wetu wa pamoja.”

Bwana Guterres amewaeleza kuwa kwa kusongesha ujume huo, “tutaweza kufanikisha lengo letu la kuwa na dunia bila silaha za nyuklia.”