Heko Hibakusha kwa kuchagiza dunia bila nyuklia- Guterres
Umoja wa Mataifa umesema hibakusha, ambao ni manusura wa mashambulio ya mabomu ya nyuklia huko Nagasaki na Hiroshima nchini Japan wamesalia kuwa viongozi wa amani na udhibiti wa kuenea silaha hizo nchini humo na duniani kwa ujumla.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo leo huko Nagasaki nchini Japan katika kumbukizi ya miaka 73 tangu Marekani iangushe bomu la atomiki lililoua maelfu ya watu na wengine kusalia na majeraha ya kudumu.
“Wanatambuliwa siyo kwa miji yao ambayo ilisambaratishwa, bali kwa dunia yenye amani ambayo wanaisaka,” amesema Bwana Guterres akiongeza kuwa Hibakusha wamepaza sauti zao kwa niaba ya binadamu wote na hivyo ni lazima kuwasikiliza.
Bwana Guterres amesema licha ya sauti hizo kupazwa na mikataba ya kimataifa kupitishwa ili kudhibiti kuenea kwa silaha hizo hatari, bado mataifa yanaendelea kutengeneza na kupanua umiliki wao wa silaha hizo.
“Serikali zinazomiliki silaha za nyuklia zinatumia kiasi kikubwa cha fedha kuziboresha. Zaidi ya dola trilioni 1.7 zilitumika mwaka 2017 kwenye silaha, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu kumalizika kwa vita baridi. Kiasi hicho in mara 80 zaidi ya fedha zinazohitajika kwa misaada ya binadamu duniani,” amesema Katibu Mkuu.
“Hebu Nagasaki na Hiroshima zitukumbushe kupatia amani kipaumbele kila siku, kufanya kazi za kuzuia mizozo, kuweka maridhiano na mazungumzo na kushughulikia mizizi ya mizozo na ghasia,” amesema Bwana Guterres.
Ametaka kila mtu kuazimia kuwa Nagasaki ni eneo la mwisho duniani kukumbwa na shambulio la nyuklia akisema yeye atashirikiana nao kufanikisha azma hiyo.
Shambulio la Nagasaki lilifanyika siku mbili baada ya lile la Hiroshima.