Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kimkakati kwa wakimbizi DRC kupunguzwa,kisa? Ukata

Msichana wa umri wa miaka akiwa amesimama kwenye darasa linalotumika na wakimbizi wa ndani, Ituri, DRC.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Msichana wa umri wa miaka akiwa amesimama kwenye darasa linalotumika na wakimbizi wa ndani, Ituri, DRC.

Misaada ya kimkakati kwa wakimbizi DRC kupunguzwa,kisa? Ukata

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema kutokana na ukata linashindwa kukidhi mahitaji ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na hivyo bila nyongeza ya ufadhili, litalazimika kukata mgao wa fedha na vifaa vya usaidizi kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji.

Dominique Hyde ambaye ni Mkurugenzi wa kitengo cha uhusiano wa nje UNHCR amesema hayo leo Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara yake nchini DRC na kushuhudia jinsi wakimbizi wanawake, wanaume na watoto wanahaha kuishi katikati ya machungu na vitisho, halikadhalika athari za ukosefu wa fedha za usaidizi wa kibinadamu.

Amesema wakati macho yote na masikio yameelekezwa kwenye majanga mengine makubwa kama Syria, Afghanistan na hivi sasa Ukraine, dharura nyingine, nyingi zikiwa Afrika zimeshindwa kuvutia usaidizi na rasilimali.

Hali ya ufadhili

DRC ni miongoni mwa operesheni za UNHCR ambazo hazijapatiwa ufadhili wa kutosha ambapo hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu wa 2022, ombi la ufadhili la mwaka hu ula dola milioni 225 limechangiwa kwa asilimia 19 pekee huku mahitaji yakiongezeka kila uchao.

Mwanzoni mwa mwaka huu, DRC ilikuwa inahifadhi wakimbizi na wasaka hifadhi zaidi ya 500,000 pamoja na wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 5.6.

Familia ya watu waliofurushwa makwao wakiwasili na lori kuishi na familia Beni baada ya kukimbia machafuko Ituri, DRC.
© UNHCR/Ibrahima Diane
Familia ya watu waliofurushwa makwao wakiwasili na lori kuishi na familia Beni baada ya kukimbia machafuko Ituri, DRC.

Kichocheo cha ongezeko la mahitaji

Bi. Hyde amesema mapigano kati ya jeshi la serikali, FARCD na vikundi vilivyojihami jimboni Kivu Kaskaizni vimefurusha watu wengine 160,000 kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.

“Halikadhalika, UNHCR na wadau wake huko jimboni Ituri wamesajili zaidi ya vifo 800 kutokana na mashambulizi ya kutumia silaha na mapanga kwenye jamii huku mashambulizi hayo yakifurusha watu 20,700 kutoka makwao,” amefafanua Bi. Hyde.

Hakuna mtoto mkimbizi ataweza kusoma sekondari mwaka huu

Kutokana na ukata, asilimia 82 ya wakimbizi wa ndani hawatapokea msaada wa kutosha wa malazi hivyo watalazimika kuishi kwenye makanisa, shule na viwanja vya mpira au maeneo mengine ya wazi na wengine wanaweza kuamua kurejea nyumbani licha ya hatari ya kuweza kushambuliwa na makundi yaliyojihami.

Afisa huyo wa UNHCR amekumbuka kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu ya msingi lakini, “DRC kutokana na ukata, ni asilimia 16 tu ya watoto ndio wana uwezo wa kwenda shule. Na katika viwango vya sasa vya ufadhili, UNHCR haiwezi kusaidia hata mtoto mmoja mkimbizi kwenda shule ya sekondari.”

Waasi waliojihami wanasalia katika eneo la Irumu jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
MONUSCO
Waasi waliojihami wanasalia katika eneo la Irumu jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Mshikamano na Ukraine ufanyike pia kwenye majanga mengine

Amesisitiza kuwa mshikamano wa kimataifa kwa Ukraine umepitiliza. “Tunahitaji hatua kama hizo na msaada zaidi wa fedha kwa majanga mengine duniani kote,” amesema Bi. Hyde akisema kuwa kila uchao, UNHCR na wadau wanashughulikia majanga haya, “lakini hatuwezi kufanya peke yetu. Tunatoa ombi la dharura kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua sasa, na kusaidia wale walio na mahitaji zaidi.”