Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji DRC yahusisha walinda amani wa UN, Katibu Mkuu Guterres ahimiza hatua zichukuliwe 

walinda amani kutoka Uruguay nchini DRC wakifanya doria katika mji wa Pinga baada ya waasi kuondoka (MAKTABA).
UN Photo/Sylvain Liechti
walinda amani kutoka Uruguay nchini DRC wakifanya doria katika mji wa Pinga baada ya waasi kuondoka (MAKTABA).

Mauaji DRC yahusisha walinda amani wa UN, Katibu Mkuu Guterres ahimiza hatua zichukuliwe 

Masuala ya UM

Katibu Mkuu António Guterres, kwa mujibu wa Naibu Msemaji wake, "amekasirishwa" na "tukio baya" la mauaji lililotokea leo Jumapili asubuhi kwenye mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Huko Kasindi, jimbo la Kivu Kaskazini, wanajeshi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Amani katika DRC, MONUSCO) wamefyatua risasi walipokuwa wakirejea kutoka mapumzikoni nchini mwao. 

Taarifa za Habari zimesema kuwa wanajeshi hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameua watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa. 

"Katibu Mkuu amesikitishwa na kuhuzunishwa na vifo na majeraha mabaya yaliyopatikana wakati wa tukio hili." Taarifa iliyotolewa jioni ya Jumapili hii kwa saa za New York, Marekani na Farhan Haq ambaye ni Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu, imeeleza. 

Bwana Guterres pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizoathirika, watu na serikali ya DRC na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.   

'Sababu zisizoeleweka' 

Katika taarifa, Mwakilishi Maalum  wa Katibu Mkuu nchini DRC ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita, amesema kuwa askari wa Kikosi cha Kujibu Mashambulizi  cha MONUSCO wamefyatua risasi katika kituo cha mpaka kwa "sababu zisizoeleweka". 

"Tukio hili la kutisha limesababisha vifo na majeraha makubwa." Amesema Keita akiwa ameshitushwa na kusikitishwa ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathiriwa na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.  

Anzisha uchunguzi 

Wakati huo huo, Katibu Mkuu ameeleza kwa msisitizo, haja ya "kuanzisha uchunuguzi kwa ajili ya uwajibikaji kwa matukio haya". 

Umoja wa Mataifa umeanzisha mawasiliano na nchi wanayotoka walinda amani, kwa lengo la "kuanzisha haraka mashauri ya kimahakama kwa kushirikisha waathiriwa na mashahidi ili hatua sitahiki ziweze kufanyika". 

Akielezea tabia ya askari hao kama "isiyoelezeka na isiyowajibika," mkuu wa MONUSCO, Bi. Keita amesema kuwa wahalifu walitambuliwa na kukamatwa kusubiri hitimisho la uchunguzi ambao tayari umeanza kwa ushirikiano na mamlaka ya DRC. 

Katibu Mkuu ameupokea uamuzi wa Mkuu wa MONUSCO wa kuwakama walinda amani wa MONUSCO wanaohusika na  hatua ya kuanzisha uchunguzi mara moja.