Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Beni, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC

Katibu Mkuu UN alaani mashambulizi ya hivi majuzi ya kundi lenye silaha mashariki mwa DRC 

© UNICEF/Arlette Bashizi
Beni, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Kivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC

Katibu Mkuu UN alaani mashambulizi ya hivi majuzi ya kundi lenye silaha mashariki mwa DRC 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuchunguza mashambulizi mabaya ya hivi karibuni yanayodaiwa kufanywa na kundi la waasi la M23.

Bwana Guterres amelaani vikali mashambulizi hayo yaliyotokea tarehe 29 na 30 Novemba katika vijiji vya Kishishe na Bambo, vilivyoko katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, katika eneo lenye hali tete la mashariki mwa nchi hiyo. 

Takriban raia 131 waliuawa, wakiwemo wanawake 17 na watoto 12, na wengine wanane walijeruhiwa. 

Uchunguzi na hatua 

"Katibu Mkuu anatoa salamu zake za rambirambi kwa familia za waathiriwa na anawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa. Anakaribisha uamuzi wa mamlaka ya DR Congo kuchunguza matukio haya kwa nia ya kuwafikisha mahakamani wale watakaobainika kuhusika." Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu alisema katika taarifa yake, Ijumaa. 

Wakati huo huo, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini DRC, na operesheni yake ya kulinda amani huko, MONUSCO, itaendelea kuunga mkono serikali katika juhudi hizi. 

Maliza uhasama sasa 

"Katibu Mkuu anawataka M23, na makundi mengine yote yenye silaha kusitisha mara moja uhasama na kupokonya silaha bila masharti." iliendelea taarifa hiyo. 

Bwana Guterres pia alitoa wito kwa pande zote kuwezesha ufikiaji wa kibinadamu kwa jamii zilizoathiriwa na kuhakikisha ulinzi wa raia na heshima kwa sheria za kimataifa za kibinadamu. 

Pia Katibu Mkuu amesisitiza dhamira inayoendelea ya Umoja wa Mataifa ya kuunga mkono serikali ya DRC na watu katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo. 

Mashambulizi hayo ni ya hivi punde zaidi katika msururu wa ghasia zilizofanywa na makundi yenye silaha dhidi ya raia mashariki mwa DRC. 

Mapema Ijumaa, Mkuu wa MONUSCO Bintou Keita alitoa taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani ambapo aliwaambia mabalozi kwamba hali ya usalama mashariki mwa DRC "imezorota sana" katika wiki zilizopita. 

TAGS: DRC, M23, MONUSCO, Bintou Keita