Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio dhidi ya walinda amani linaweza kuwa uhalifu wa kivita, walioshambulia MONUSCO wafikishwe kwenye sheria - Guterres 

Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.
UN Photo/Martine Perret
Walinda amani wakifanya doria huko Butembo, Kivu Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili kuhakikisha usalama wa jamii.

Shambulio dhidi ya walinda amani linaweza kuwa uhalifu wa kivita, walioshambulia MONUSCO wafikishwe kwenye sheria - Guterres 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali shambulio baya lililotokea jana tarehe 26 Julai huko Butembo, jimbo la Kivu Kaskazini dhidi ya askari wa kulinda amani wanaohudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuleta utulivu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO). 

Taarifa iliyotolewa jijini New York Marekani na Farhan Haq ambaye ni Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, imeeleza kuwa maafisa wawili wa polisi raia wa India na mwanajeshi mmoja wa Morocco wameuawa katika tukio hilo, huku polisi mmoja wa Misri akijeruhiwa wakati wa maandamano yenye vurugu kwenye kituo cha MONUSCO.  

“Katibu Mkuu ametoa pole kwa familia za walinda amani walioaga dunia, pamoja na Serikali na watu wa India na Morocco. Anamtakia ahueni ya haraka askari wa kulinda amani aliyejeruhiwa.” Imesema taarifa ya Farhan Haq.  

Katibu Mkuu pia analaani vikali ghasia zinazolenga vituo kadhaa vya Umoja wa Mataifa katika jimbo la Kivu Kaskazini tangu tarehe 25 Julai, ambapo watu binafsi na makundi waliingia kwa nguvu katika ngome na kuhusika katika uporaji na uharibifu wa mali ya Umoja wa Mataifa, huku pia wakipora na kuchoma moto makazi ya Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, imeeleza taarifa na kuongeza kuwa, “Katibu Mkuu anasikitika kupoteza maisha ya waandamanaji katika muktadha huu na anathibitisha kujitolea kwa MONUSCO kufanya kazi na mamlaka ya DRC kuchunguza matukio haya.”   

Aidha Katibu Mkuu amekumbushia makubaliano ya Hali ya Vikosi yaliyohitimishwa kati ya Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo yanahakikisha unyeti kwa majengo ya Umoja wa Mataifa. Anasisitiza kwamba shambulio lolote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa uhalifu wa kivita na kutoa wito kwa mamlaka ya DRC kuchunguza matukio haya na kuwafikisha haraka mbele ya sheria wale waliohusika. Hadi kufikia hapo, Katibu Mkuu anakaribisha kauli ya Msemaji wa Serikali ya DR Congo, iliyotolewa tarehe 25 Julai, iliyolaani ghasia hizo na kuashiria kuwa wahusika watachukuliwa hatua. 

Katibu Mkuu anasisitiza dhamira ya dhati ya Umoja wa Mataifa kwa uhuru, umoja na utimilifu wa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba Umoja wa Mataifa kupitia Mwakilishi wake Maalum katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ujumbe wake ulioaidhinishwa na Baraza la Usalama, wataendelea kuunga mkono Serikali ya DRC na watu wake katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo.