Skip to main content

Licha ya vikwazo, WFP yaendelea kuokoa maisha Haiti 

Vurugu za magenge mjni Port-au-Prince, Haiti, zinawatia hofu watu wazima na watoto vile vile.
UNDP Haiti/Borja Lopetegui Gonzalez
Vurugu za magenge mjni Port-au-Prince, Haiti, zinawatia hofu watu wazima na watoto vile vile.

Licha ya vikwazo, WFP yaendelea kuokoa maisha Haiti 

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Haiti, ambako karibu nusu ya idadi ya watu tayari hawana uhakika wa chakula, njaa inatazamiwa kuongezeka huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei, gharama kubwa za chakula na mafuta na kuzorota kwa usalama, linaonya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP ingawa linaendelea kutoa msaada kwa Wahaiti walio katika mazingira hatarishi.

 

Arnold Kayanda/UNNewsKiswahili
Licha ya vikwazo vya magenge ya uhalifu, WFP yaendelea kuokoa maisha Haiti

Kupitia video zilizochukuliwa kutoka angani zikionesha Port-au-Prince, mji mkuu wa Haiti ulivyo tulia ufukweni mwa kisiwa hicho kinachopakana na Jamhuri ya Dominican katika bahari ya Caribea, ni vigumu kwa mtu kujua kuwa hali si shwari ndani ya Haiti hadi unaposhuka chini mitaani. 

Ni maandamano. Wengine wamebeba mabango, wengine bendera na wengine matawi ya miti. Wanadai amani na usalama dhidi ya vurugu za magenge ya uhalifu. 

Polisi wameweka vizuizi vya ukaguzi lakini katika baadhi ya maeneo yanayosemwa kuwa ngome za magenge, unaweza kusikia milio ya risasi mchana kweupe.  

Kwingine watu wanaonekana wamekusanyika  kwenye vituo vya mafuta na midumu. Uhaba wa mafuta unaosababishwa na magenge ya wahalifu kukata njia kuu za kufikia Port au Prince sasa unachangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta duniani kote kutokana na mgogoro wa Ukraine. Vituo vingine hata vimefungwa kwa kukosa mafuta. 

Licha ya vikwazo, WFP nchini Haiti imekuwa ikiisaidia Serikali kwa misaada ya kibinadamu na maendeleo ili kukabiliana na chanzo cha njaa na inapanga kuwasaidia watu milioni 1.7 mwaka huu wa 2022. WFP inaimarisha mnepo wa Wahaiti na kuimarisha ulinzi wa kijamii na mifumo ya chakula. Jean-Martin Bauer ni Mkurugenzi wa WFP nchini Haiti anasema, "kwanza kabisa magenge na athari zao katika biashara ya masoko na maisha vimesababisha ongezeko la uhaba wa chakula. Bei za juu za vyakula za kimataifa pia zinachangia janga la chakula hapa nchini. Ili kutatua, WFP imezindua huduma ya baharini, tuna feri inayochukua misaada kutoka hapa hadi katika maeneo mengine ya nchi. Pia tuna huduma ya anga, helikopta inayosafirisha misaada kutoka hapa  hadi sehemu zote za Haiti.” 

Ingawa WFP inajitahidi kuokoa maisha, kwa muda wa miezi sita ijayo, inakabiliwa na upungufu wa ufadhili wa dola za Marekani milioni 39 kwa ajili ya kutimiza shughuli zake nchini Haiti. 

TAGS: Haiti, WFP, Njaa