Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko Haiti 2010 lilikuwa pigo kubwa kwa Umoja wa Mataifa.

Picha ya juu ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince
MINUJUSTH/Leonora Baumann
Picha ya juu ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince

Tetemeko Haiti 2010 lilikuwa pigo kubwa kwa Umoja wa Mataifa.

Msaada wa Kibinadamu

Nusu ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince uliharibiwa, watu 220,000 waliripotiwa kupoteza maisha na wengine milioni 1 walipoteza makazi. Hili lilikuwa pigo la tetemeko la ardhi lililoipiga nchi ya Haiti tarehe 12 mwezi Januari mwaka 2010.

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa Haiti waliathirika na kati yao wapatao 102 akiwemo mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Hédi Annabi pamoja na naibu wake Luiz Carlos da Costa walipoteza maisha.

Rais wa wakati huo wa chama cha wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa Stephen Kisambira alisema “ni pigo kubwa kuwahi kutokea kwa wakati mmoja katika historia ya Umoja wa Mataifa katika kutunza amani”

Mmoja wa manusura ni Sophie Boutaud de la Combe ambaye hivi sasa ni mkuu wa mawasiliano katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya usaidizi wa haki huko Haiti MINUJUSTH, wakati wa tukio alikuwa mjamzito wa miezi 7 na siku chache tu akikaribia kwenda mapumziko.

Jengo alilokuwemo lilibomoka lote lakini Bi de la Combe aliweza kutoroka kupitia ukuta uliovunjika. Kwa saa nyingi, yeye pamoja na manusura wenzake walipekua katika kifusi kujaribu kutafuta wengine ambao walikuwa bado wamekwama chini ya jengo. Siku mbili baadaye Sophie Boutaud de la Combe alilazimika kuondoka Haiti katika hali ambayo anaieleza kuwa ni ya kusikitiza kwani alitaka kuusaidia Umoja wa Mataifa na watu wa Haiti. Baadaye alirejea nchini Haiti mnamo mwaka 2013 akifurahi kushiriki katika kuijenga upya Haiti na kuwaenzi wenzake waliopoteza maisha.

Umoja wa Mataifa ulipoadhimisha miaka 6 ya tukio la tetemeko la ardhi lililoua wahaiti 250,000 na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wapatao 102. Maadhimisho haya yalifanyika mwaka 2016.
MINUSTAH
Umoja wa Mataifa ulipoadhimisha miaka 6 ya tukio la tetemeko la ardhi lililoua wahaiti 250,000 na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wapatao 102. Maadhimisho haya yalifanyika mwaka 2016.

 

Miaka 9 baada ya tetemeko la ardhi, hali nchini Haiti ni ya tofauti. Bi dela Combe anasema serikali ya nchi hiyo hivi sasa imejiandaa kukabiliana na majanga ya asili kama hayo.

“Miezi michache iliyopita kulikuwa na tetemeko lililoathiri kaskaZini mwa nchi. Nchi ilikuwa imejiandaa na walituma watu wao kusaidia walioathirika hata bila MINUJUSTH. Halikuwa tetemeko kubwa lakini sasa watu wanajua la kufanya inapotokea hali kama hiyo. Na muhimu zaidi tunasikia mara kwa mara ilivyo muhimu kujenga vizuri, kwa uimara ili tetemeko litakapotokea lisihatarishe maisha”