Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari za uongo, upotoshaji na matamshi ya chuki vinatumika kama silaha za vita: Guterres

Mitandao ya kijamii inaewza kuchochea kusambaa kwa taarifa potofu kuhusu COVID-19
Unsplash/Redgirl Lee
Mitandao ya kijamii inaewza kuchochea kusambaa kwa taarifa potofu kuhusu COVID-19

Habari za uongo, upotoshaji na matamshi ya chuki vinatumika kama silaha za vita: Guterres

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa - UN umesema umeimarisha mawasiliano ya kimkakati katika operesheni za ulinzi wa amani duniani kote ili kukabiliana na taarifa za upotoshaji au uongo zinazoenezwa hususan mitandaoni.  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mjadala wa ngazi za juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani amesema taarifa za uongo au upotoshaji ni hatari sana kwa walinda amani kwani mbali na kuhatarisha Maisha yao pia zinaweza kutumika kujenga chuki baina ya walinda amani na jamii wanazolinda ndio maana UN unaamini mawasiliano ni muhimu sana. 

Guterres amesema “Kama nilivyosema nilipoapishwa kuwa katibu Mkuu wa UN mwaka 2016 lazima tuweza kuwasiliana vyema kuhusu kile tunachofanya, kwa njia ambazo kila mtu anaelewa.”

Hata hivyo ameeleza pamoja na UN kuwa na mkakati kabambe wa mawasiliano ulimwenguni kunahitajika mageuzi makubwa ya kimkakati ya mawasiliano ili kuboresha zana na majukwaa ya kuwafikia watu ulimwenguni kote kwakuwa kazi ya shirika hilo sit u kufahamisha ulimwengu bali pia kushirikisha hadhira katika kuunga mkono dhamira muhimu ya Umoja wa Mataifa. 

Walinda amani wa MINUSMA wakiwa katika doria eneo la Aguelhok nchini Mali
© MINUSMA/ Harandane Dicko
Walinda amani wa MINUSMA wakiwa katika doria eneo la Aguelhok nchini Mali

Vita vya sasa si vya silaha pekee

Mazingira ambayo walinzi wa amani wanafanya kazi ni hatari zaidi sasa ikilinganisha na miaka ya nyuma ameeleza mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, mivutano ya kijiografia na kisisasa katika ngazi za kimatfia imekuwa ikijirudia ndani ya nchi zenyewe hali inayofanya migogoro hiyo kuwa migumu zaidi na kujaa mikanganyiko. 

Ameeleza mifarakano ya kimataifa imezidi kuwa mingi ambayo pia huleta athari mpaka ndani ya nchi, “Walinda amani wanakabiliana na magaidi, wahalifu, makundi yenye silaha na washirika wao ambao wengi wanaweza kupata silaha za kisasa zenye nguvu na wengi wenye nia ovu ya kuendeleza machafuko kwakuwa yanawanufaisha lakini silaha wanazotumia si bunduki na vilipuzi tu, wanatumia habari za uongo, upotoshaji na matamshi ya chuki kama silaha za vita.” Amebainisha Guterres

Ameongeza kuwa lengo la kufanya hivyo lipo wazi, ni kudhalilisha wale wanaitwa “wengine”, kutishia jamii zilizo hatarini pamoja na walinda amani wenyewe na hata kujipa uhalali wa kufanya ukatili. 

“Nikutokana na sababu hizo ndio maana “mawasiliano ya kimkakati ni muhimu katika wigo wa mamlaka yetu ya kulinda amani na kufikia dhamira ya Umoja wa Mataifa ambayo pamoja na mambo mengine tuna jukumu la kulinda raia, kuzuia vurugu, kusitisha mapigano, kuendeleza ajenda ya wanawake na mambo mengine mengi.”

Ameeleza utafiti uliofanywa na UN hivi karibuni umebainisha nusu ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaona habari za upotoshaji zinaathiri utekelezai wa mamlaka na kutishia usalama wao. 

Akitolea mfano wa athari ya Habari za uongo ameeleza “Tunaona matukio zaidi na zaidi ambapo habari za uwongo huenea kama moto wa nyika, zikizuia walinda amani wetu kutekeleza kazi yao ya kuokoa maisha na kubadilisha maisha. Kwa kutoa mfano mmoja tu: Nchini Mali, barua ya uwongo iliyodai kuwa walinzi wetu wa amani walikuwa wakishirikiana na makundi yenye silaha iliwekwa kwenye mtandao wa Facebook. Ilisambaa kwenye WhatsApp na ikachukuliwa na vyombo vya habari vya kitaifa. Barua hii ya uwongo ilichochea uhasama na chuki dhidi ya walinda amani wetu, na kuifanya kazi yao muhimu ya kulinda raia kuwa ngumu zaidi.”

Serikali na makampuni ya intaneti wameshindwa kuzuia chuki mtandaoni
Unsplash/Priscilla du Preez
Serikali na makampuni ya intaneti wameshindwa kuzuia chuki mtandaoni

Nini kinafanyika

Mawasiliano ya kimkakati na yakuaminika, sahihi, na yanayolenga binadamu ni mojawapo ya zana bora na za gharama nafuu za kukabiliana na tishio la uenezaji wa habari za upotoshaji kwakuwa mawasiliano ya njia mbili  hujenga uaminifu na pia uungwaji mkono wa kisiasa na wa umma kwa ujumla.

Umoja wa Mataifa una maeneo sita madhubuti ya kusaidia kuboresha mawasiliano ya kimkakatia ambayo ni:-  

1.    Wafanyakazi walio kwenye misheni wale na wanajeshi au sio wanajeshi kuwa na ujuzi katika mawasiliano ya kimkakati lengo likiwa kukuza mtandao wa mawasiliano mashinani.  Nchi zinazotoa wanajeshi wake kushiriki katika misheni zinahimizwa kuhakikisha wafanyakazi wake wana stadi hizo .

2.    Viongozi wa misheni wanajukumu na wajibu wa kuongozo mawasiliano ya kimkakati katika maeneo yao na kuhakikisha yanajumuishwa katika vipengele vyote wakati wa mipango na wanapofanya maamuzi. 

3.    Umoja wa Mataifa unatoa mafunzo na miongozo inayojumuisha ukusanyaji na ushirikishaji wa mbinu bora. 

4.    Tunafanya kazi na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni ya teknolojia na vyombo vya habari, na nchi Wanachama ili kutambua na kutumia zana bora zaidi za kutambua na kupinga upotoshaji wa taarifa na matamshi ya chuki.

5.    Tunaendelea kufuatilia na  kufanya tathmini ya ufanisi wa kampeni zetu za taarifa ili kuhakikisha tunafanya marekebisho pale inapohitajika kurekebisha mkakati wetu kulingana na mahitaji ya kimbinu ya muktadha mahususi tunayofanyia kazi.

6.    Na mwisho tunaendelea kupeleka mawasiliano ya kimkakati ili kuimarisha uwajibikaji na kuunga mkono juhudi za kukomesha tabia mbaya ya wafanyakazi na washirika wet ikiwa ni pamoja na kupiga vita unyanyasaji na unyanyasaji wa kingono.