Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimesikitishwa sana na mauaji ya kutisha ya Shinzo Abe – António Guterres 

Katibu Mkuu Antonio Guterres  na waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari Tokyo. Agosti 2018.
UN Dan Powell
Katibu Mkuu Antonio Guterres na waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari Tokyo. Agosti 2018.

Nimesikitishwa sana na mauaji ya kutisha ya Shinzo Abe – António Guterres 

Masuala ya UM

Muda mfupi baada ya Japan kutangaza kifo cha Waziri Mkuu wake wa zamani, Shinzo Abe, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter ameeleza kusikitishwa sana na mauaji hayo ya kutisha. 

Abe amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa jukwaani katika shughuli za kisiasa alipokuwa akikifanyia kampeni chama chake katika mji wa kusini wa Nara. 

“Nilikuwa na fursa ya kumfahamu kwa miaka mingi na nitakumbuka ushirikiano wake na kujitolea kwake kwa ushirikiano wa mataifa.” Ameandika Guterres.  

Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi, “kwa familia yake, watu na Serikali ya Japan.” 

Baadaye kupitia taarifa iliyotolewa jijini New York Marekani kupitia kwa Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu, ameeleza namna Katibu Mkuu Guterres anakumbuka dhamira ya Shinzo Abe ya kukuza amani na usalama, kupigania Malengo ya Maendeleo Endelevu na kutetea huduma ya afya kwa wote.  

“Akiwa Waziri Mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi, alijitolea kufufua uchumi wa nchi yake na kuwatumikia watu wa Japan.” Imeeleza taarifa hiyo. 

Aidha taarifa hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kitendo hicho kilichoishangaza sana jamii ya Japan, nchi yenye viwango vya chini vya uhalifu wa kutumia bunduki imeeleza kuwa Abe atakumbukwa kama mtetezi shupavu wa ushirikiano wa kimataifa, kiongozi anayeheshimika, na mfuasi wa Umoja wa Mataifa. 

Vyombo vya habari vya Japan vinadai walioshuhudia tukio hilo wamemshuhudia mtu mmoja kwa jina Tetsuya Yamagami akimfyatulia risasi Bwana Abe mara mbili na risasi zote zimempata na kusababisha jeraha kubwa katika maeneo ya shingoni na kwingine katika mwili karibu na shingo.