Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana waenzi stadi ya ‘Inamura no Hi’ iliyotumika miaka 164 kupunguza janga la tsunami Japan

Madhara ya Tsunami na tetemeko Indonesia yaliwaacha wengi bila makazi.
UNICEF/Arimacs Wilander
Madhara ya Tsunami na tetemeko Indonesia yaliwaacha wengi bila makazi.

Vijana waenzi stadi ya ‘Inamura no Hi’ iliyotumika miaka 164 kupunguza janga la tsunami Japan

Tabianchi na mazingira

Mkuu wa ofisi  ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupunguza athari za majanga, UNISDR, Mami Mizutori amewaeleza wanafunzi wanaokutana katika kongamano la kukuza uelewa kuhusu Tsunami kuwa kupunguza hatari za majanga ni eneo muhimu ambalo linahusu kila taaluma.

Kongamano hilo lilikutanisha wanafunzi wa vidato vya juu kwa ajili ya siku ya kukuza ufahamu kuhusu Tsunami hii leo, limewakutanisha wanafunzi 379 kutoka nchi 48 ikiwemo Japani na linafanyika jimboni

Wakayama, nchini Japan, nchi ambayo inatambulika kwa uwezo wake na maarifa ya kudhibiti hatari zinazoweza kusababishwa na Tsunami.

Bi. Mizutori amesema ana matumaini kuwa taaluma yoyote ambayo mwanafunzi ataichukua katika siku za usoni, itatoa kipaumbele katika masuala ya kupunguza hatari za majanga na watakuwa mabalozi wa suala hili.

Kongamano hilo limefanyika kwenye eneo ambako mnamo tarehe 5 Novemba mwaka 1854, mkulima wa mpunga Hamaguchi Goryo alitia moto vitita vya mpunga wake kama tahadhari kwa wanakijiji wenzake kuwa Tsunami ilikuwa inakuja na hivyo akawaokoa wengi. 

Aina hiyo ya utoaji wa tahadhari inaitwa ‘Inamura no Hi’ kwa lugha ya kijapani ambapo wanafunzi wamepitisha azimio la Inamura ho Hi wakati huu ambapo madhara ya tsunami iliyokumba Indonesia bado iko kwenye fikra za watu wengi.

Azimio lililopitishwa na wanafunzi limeorodhesha umuhimu wa kulinda uhai, kujenga upya mnepo kwa majanga ya siku za usoni.

Pia wanafunzi hao walikula kiapo cha kuenzi ari ya Hamaguchi Goryo na kutekeleza mafunzo waliyoyapata katika kongamano hilo kuokoa maisha katika nchi zao.

Katika ujumbe uliotumwa kwa njia ya video, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema, “ninatumai ninyi nyote mtarithi ari ya Goryo Hamaguchi na mtakuwa viongozi katika wa siku za usoni katika kuzuia majanga. Ni matumaini yangu kuwa kongamano hili litakuwa muongozo kwa maisha ya wengi kuokolewa kwa vizazi vijavyo”