Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pamoja na changamoto za uhaba wa walimu na nyenzo za kufundishia, Uganda yadhamiria kukuza Kiswahili

Wanafunzi waliovaa sare za shule wamekaa kwenye madawati ya mbao darasani, wakiandika kwenye madaftari kwa kalamu.
UN News/John Kibego Wanafunzi katika shule ya St. Maliko Uganda.

Pamoja na changamoto za uhaba wa walimu na nyenzo za kufundishia, Uganda yadhamiria kukuza Kiswahili

Utamaduni na Elimu

Kuelekea maadhimisho ya pili ya siku ya lugha ya Kiswahili duniani julai 7 wananchi wa Uganda wanafanya kila juhudi kuhakikisha wanazungumza na kuelewa vyema lugha hiyo na kufuta usemi wa utani wa mitaani kuwa Kiswahili kimezaliwa Tanzania, kikafia Kenya na kuzikwa Uganda. 

Mwandishi John Kibego ametembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na wananchi, wanafunzi na viongozi kufahamu namna wanavyohakikisha Kiswahili kinazungumzwa vyema. 

Usafiri wa umma

Katika eneo la Main Street jijini Hoima kuna kituo cha waendesha pikipiki maarufu bodaboda kundi la vijana wamekaa wakisubiri wateja na mmoja kati yao ni Joel ambaye anaeleza kuwa wateja wanapokuja eneo hilo kutaka usafiri ikiwa wanazungumza lugha ya Kiswahili basi yeye ndio huzungumza nao kwani wenzake hawajui kuzungumza Kiswahili.

“Nilijifunza Kiswahili sababu ya kazi zangu, mimi muda mwingine nafanya kazi kwenye bus la abiria au bodaboda na huko ndio nilikojifunzia kwani nilikuwa nasafiri naenda mbali kabisa kupeleka mizigo kama mbao au mahindi.” 

Anaendelea kusema amekuwa muhamasishaji mzuri wa kuzungumza lugha hiyo lakini wenzake wamekuwa wakipinga. “mimi ninapokuwa nazungumza wao (wenzake) wanacheka tu na kucheka.”

Mteja anapokuja wenzake kwakuwa hawajui kuzungumza lugha hiyo hujadili tu fedha kiasi gani basi “lakini mimi najua na naweza kuzungumza na mteja na kumchukua”

Mwalimu katika shule ya St. Maliko nchini Uganda anaandika ubaoni akiwa na somo la lugha ya Kiswahili.
UN News/John Kibego CrissyI Rumba, Mwalimu katika shule ya St. Maliko nchini Uganda.

Mashuleni

Baada ya kuzungumza na Joel, Kibego alifunga safari kwenda kutembelea shule ya sekondari ya St Maliko marufu kama St Mark. ambako huko alikuta mafunzo yanaendelea kwenye darasa la kidato cha kwanza. 

Mwalimu Crissy Irumba akiwafundisha kutoa salam kwa lugha ya Kiswahili “Hali kwa sasa ni nzuri sana kwani wanafunzi wanajifunza na wanafurahi kujua lugha ya Kiswahili” 

Mwalimu Irumba aliyeanza kufundisha somo la Kiswahili mwaka 2018 anasema wanakabiliwa na upungufu wa walimu wa lugha hiyo ndio maana anafundisha shule nne tofauti. 

Katika shule zote anazofundisha anasema changamoto anayokutana nayo kubwa ni wanafunzi kutaka kufundishwa kwa lugha mama. “watoto hawa shule za msingi hawakufundishwa Kiswahili hivyo nalazimika kuwafundisha kwa lugha ya kiingereza ili wanielewe vizuri namaanisha nini na pia natumia lugha mama ya Kinyoro.”

Mafanikio yameanza kuyaona kwani wanafunzi wanapenda sana somo hilo na pia wanavitabu vya kutosha vya kufundishia. 

“Ushauri wangu tu kwa serikali ni waaanze kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu.” Ameeleza pale alipoulizwa nini kifanyike kukuza lugha hiyo nchini Uganda. 

Wanafunzi waliokutwa wakifundishwa Kiswahili wameeleza furaha yao kwa kusoma somo hilo na kueleza wameanza kuzungumza wakiwa kidato cha tano lakini wanafuraha sana kwani wanaweza kuelewa na kuzungumza na wengine. 

Miongoni mwa wanafunzi hao wengine wamesema wanatamani hapo baadae wawe walimu wa somo la Kiswahili.

Herriet Karing, mwalimu katika shule ya serikali huko Hoima, Uganda, ameketi kwenye dawati lake.
UN News/John Kibego Herriet Karing, Mwalimu katika shule za serikali Hoima Uganda.

Takwa la serikali la kufundisha Kiswahili

Kwenye shule ya msingi ya Hoima Public Bi Haririet Karungi ni mwalimu Mkuu na ameeleza kuwa serikali inataka shule zote wafundishe lugha ya Kiswhaili na iliwapatia vitabu vya kufundishia. 

Hata hivyo ameeleza wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kufundisha Kiswahili rahisi hata cha darasa la nne kwani wengi wa walimu waliosoma zamani hawakufundishwa Kiswahili vyuoni kwa hiyo hawawezi kufundisha watoto.

“Walimu wapya nao wanaohitimu unapoangalia na kufanya utafiti, unapata kwamba wamefunzwa Kiswahili chuoni lakini wanapokwenda kwa mafunzo kabla ya kuhitimu, hawajaribiwi kukifundiha. Inamaanisha hata chuoni hakijatiliwa manane isipokuwa kuwafunza tu kwa sababu kipo lakini sio kuwandalia nao wafundishe watoto”

Mwalimu huyo Mkuu anasema alijaribu kupata mwalimu lakini kwa sababu alikuwa akitoka kwenye shule za binafsi alikimbia alipopata malipo bora zaidi. 

“Alikwenda kupata malisho yaliyo kijani zaidi. Tulijaribu kama shule kupata mwalimu afundishe angalau kwenye darasa la nne na la tano lakini kwa sasa hatuna”

Ameiomba serikali ya kati kuzingatia walimu wanaofundishwa kiswahili chuoni kwa ngazi ya diploma na kuwahimiza walimu watekeleze wanapohitimu. 

Nao pia walimu waliosoma zamani ameomba wapangiwe kusoma kozi fupi za lugha ya Kiswahili”

Serikali ya Uganda inafanya nini kukuza kiswahili?

 Johnson Kusiima Biagana ni Mkaguzi Mkuu wa Elimu wa jiji la Hoima na anasema katika kile anachokiona ni moyo wa kukuza ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, serikali ya Uganda ilitangaza Lugha ya Kiswahili ifundishwe kwa lazima kwenye tasisi zote za elimu kote nchini. 

Uamuzi huo ni bora kwa sababu kwa nchi za Afrika Mashariki, Uganda anaona wanafanya vibaya kuhusiana na lugha ya Kiswhaili.

Biagana amekiri changamoto iliyoelezwa na walimu ya uhaba wa walimu wenye ujuzi wa kufundiha lugha ya Kiswahili hususan katika shule za msingi. 

“Serikali ya Uganda kupitia wizara ya afua inafahamu changamoto hii. Inafanya juu chini kuona kwamba imepata wakandarasi wa kuchapisha vitabu ili viletwe mashuleni na pia walimu wapatiwe ujuzi wa kufundisha Kiswahili haraka iwezekanavyo ili Kiswahili kifundishwe kama lugha”

Johnson pia amewapongeza walimu wanaoendelea kufundisha lugha hiyo kwa wanafunzi na kusema “Hata kama si wataalamu wa kufundisha lugha ya Kiswahili, kwa kiasi fulani wametusaidia kufundisha watoto wetu hapa kwani Bunyoro kuna makabila mengi. Huu ni mji muhimu wa mafuta na hivyo watu wengi mno sio tu Wanyoro lakini watu kutoka hata DRC Hamna mtu kutoka DRC ataongea Kinyoro chako. Tukifunza watu wetu kuongea Kiswahili, tutaweza kuongea kimataifa”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO limetenga tarehe 07 Julai kila mwaka kuwa siku ya lugha adhimu ya Kiswahili. 

Taarifa hii imeandikwa na John Kibego