Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukilinda misitu itatulinda tukiharibu tunajiharibia wenyewe: Guterres

Misitu hufunika 93% ya ardhi ya Suriname na ina wingi wa viumbe hai.
UNDP Suriname/Pelu Vidal
Misitu hufunika 93% ya ardhi ya Suriname na ina wingi wa viumbe hai.

Tukilinda misitu itatulinda tukiharibu tunajiharibia wenyewe: Guterres

Tabianchi na mazingira

“Ulinganisho ni rahisi, kama tukilinda misitu yetu nayo itatulinda. Kama tukiharibu misitu yetu tunajiaribia wenyewe.” Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyoitoa hii leo nchini Suriname akiwa ziarani nchini humo. 

Katibu Mkuu Guterres akiwa nchini humo amejionea jinsi taifa hilo linavyohifadhi misitu yake na kupongeza uongozi wa taifa hilo ambapo takriban asilimia 93 ya taifa hilo limezingirwa na misitu ya mvua. 

Sehemu kubwa ya eneo la pwani ya Suriname ni ya hali ya chini na huathiriwa na majanga ya asili.
UNDP Suriname/Pelu Vidal
Sehemu kubwa ya eneo la pwani ya Suriname ni ya hali ya chini na huathiriwa na majanga ya asili.


Watu wa asili wanaongoza katika utunzaji wa uoto wa asili

Akizungumzia kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa ukataji miti unaongeza hatari zaidi duniani kwakuwa unaleta ukame na pia kusababisha moto kwenye misitu. 

Athari nyingine kubwa ni moshi wa viwandani ambao unasababisha uharibifu kwenye tabaka la ozoni na wachangiaji wakubwa wa uharibifu huu ni nchi tajiri ambapo ameeleza mchi tajiri zaidi au G7 zinachangia asilimia 80 ya uharibifu huo.

Akizungumza baada ya kutembelea watu wa asili wa Suriname na kuona namna wanavyolinda misitu pamoja na kutunza mikoko ili maji ya baharí yasiharibu ardhi ya taifa hilo Guterres amesema “Nilichokiona Suriname kinanipa matumaini na msukumu, lakini tunachokiona kote ulimwenguni kinatupa mshtuko na hasira kwakuwa kuna ukataji miti uliokithiri na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi hali inayo udhi na kutia aibu. Ni dunia kujiua kwa mwendo wa polepole” 

 

Kilimo ni muhimu kwenye uchumi wa Suriname
UNDP Suriname
Kilimo ni muhimu kwenye uchumi wa Suriname

G7 lipeni fidia 

Watu wa asili hawajachangia mabailiko ya tabianchi hata hivyo wao ndio miongoni mwa watu wanaoathirika zaidi. Hata hivyo wana majawabu ambayo ulimwengu unaweza kujifunza mengi kutoka kwao. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres ameyakumbusha mataifa tajiri kutimiza wajibu wao wa ahadi ya kutia dola bilioni 100 kwa mwaka kwa ajili ya hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. 

“Suluhu zinazotegemea asili kama vile kuhifadhi mikoko, misitu ya mvua na mifumo mingine ya ikolojia ni muhimu. Ulimwengu unahitaji zaidi mipango kama hii. Katika nyanja zote ni muhimu mataifa haswa yale tajiri zaidi, yafanye kazi pamoja kupunguza ongezeko la joto ulimwenguni hadi kudikia digrii 1.5 katika viwango vya Sentigredi na kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ya tabianchi yajayo.”

Amesema shida nyingi za mabadiliko ya tabianchi ni kutokana ni kutokana na kushindwa kuwepo na uongozi mzuri hasa unaosimamia mabadiliko ya tabianchi tofauti na nchini Suriname ambao uongozi umeongoza njia bora na sasa watu wa taifa hilo wanafurahia uoto wa asili na misitu pamoja na ulindaji wa tabaka la ozoni. 

Dunia yetu inaelekea kwenye mwelekeo mbaya. Sayansi ipo wazi , ili kufikia lengo la kuwa na juzi joto 1.5C ulimwengu lazima upunguze uchafuzi wa hewa kwa asilimia 45 mpaka kufikia mwaka 2030, lakini kwa sasa ahadi zilizotolewa na mataifa yatasababisha matokeo ya kupunguza hewa chafuzi kufikia asilimia 14 pekee ifikapo mwaka 2030. 

“Kwa kila saa inayopita ya mabadiliko ya tabianchi, malengo ya kufikia nyuzi joto 1.5 hupungua na kudhoofika. Wanao ongoza kwa uchafuzi mkubwa wana jukumu maalum la kuhakikisha wanapunguza athari hizo.”

Katika taarifa yake Guterres pia ameyapongeza mataifa ya Caribbean kwakuwa mstari wa mbele kutafuta suluhisho za migogoro ya mabadililo ya tabianchi na kuonesha uongozi thabiti katika eneo hilo.