Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya tabianchi ni mbaya zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote- Guterres

Viongozi wa kundi la nchi 7,  G7 na wadau wao kwenye picha ya pamoja katika Hoteli la Palais Biarritz nchini Ufaransa,. (25 Agosti 2019)
White House/Andrea Hanks
Viongozi wa kundi la nchi 7, G7 na wadau wao kwenye picha ya pamoja katika Hoteli la Palais Biarritz nchini Ufaransa,. (25 Agosti 2019)

Hali ya tabianchi ni mbaya zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko Biarritz Ufaransa kushiriki mkutano wa kundi la nchi 7 zenye uchumi wa juu zaidi duniani, G7, ametumia fursa hiyo kuendelea kupaza sauti ya udharura wa mabadiliko ya tabianchi unaokumba ulimwengu hivi sasa.

Hali ya tabianchi hivi sasa ni mbaya kuliko ilivyokuwa tulivyokutana mjini Paris, Ufaransa na kupitisha mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, ndivyo alivyosema Katibu Mkuu Guterres alipozungumza na waandishi wa habari hii leo kandoni mwa mkutano huo wa G7.

Udharura anaosema unazingatia taarifa ya kwamba mwezi uliopita ulivunja rekodi ya kuwa mwezi wenye joto zaidi na wakati huo huo shirika la hali ya hewa duniani, WMO likisema kuwa kiwango cha hewa ya  ukaa kwenye anga ni cha juu zaidi.

Amesema kiwango cha sasa cha hewa ya ukaa angani kinafanana na miaka milioni tatu au tano iliyopita,wakati ambao kiwango cha joto kilikuwa ni cha juu sasa na maji ya usawa wa bahari yalikuwa mita kati ya 10 au 20 juu zaidi ikilinganishwa na sasa.

Guterres ametaja kuyeyuka kwa theluji kwenye ncha ya kaskazini mwa dunia na moto unaoendelea kuteketeza msitu wa mvua wa Amazon huko Amerika ya Kusini.

Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu anataka hatua zaidi za kupunguza hewa chafuzi akisema kila nchi itimize ahadi kwa mujibu wa mkataba wa Paris akisema kuwa cha kusikitisha hata ahadi zilizotolewa hazitekelezwi

“Tunahitaji hatua zaidi tunaona jamii zikihamasishana, vijana nao wakihamasishana, tunataka viongozi wa serikali wanaokuja New York, kwa ajili ya mkutano wa tabianchi mwezi ujao waweze kutoa ahadi za kina ili kupunguza hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050” amesema Katibu Mkuu.

Amekumbusha kauli yake ya nchi kuacha kutoza kodi watu na badala yake zitoze hewa ya ukaa na ziache kujenga viwanda vya makaa ya mawe baada yam waka 2020.

Bwana Guterres amesema hata hivyo uamuzi huo unataka utashi wa kisiasa na mkutano wa G7 ni fursa bora zaidi na kinachotakiwa ni mataifa hayo yaoneshe mfano.

Swali kuhusu msitu wa Amazon

Kisha waandishi wa habari walimuuliza maswali Katibu Mkuu Guterres ambapo miongoni mwa maswali ni kuhusu moto unaoendelea kuteketeza msitu wa mvua wa Amazon huko Amerika ya Kusini ambapo waandishi wa habari walitaka kufahamu iwapo ameridhishwa na ahadi zilizotolewa kwenye mkutano huo kuhusu tukio hilo.

Katibu Mkuu amesema, “naamini kwamba ni jambo muhimu sana. Kuna wito thabiti wa kutaka jamii ya kimataifa iweze kusaidia nchi za Amazoni; hivi sasa ili kuzima mioto inayoendelea na baadaye kusaidia upandaji miti kwenye msitu jambo ambalo ni muhimu sana ili kulinda eneo hilo muhimu kwa uhai wa binadamu.”

Amesema anaamini kuwa wanaweza kuhamasisha rasilimali zaidi kwa siku zijazo na kwamba utashi wa kisiasa wa nchi hizo husika uimarike zaidi. “Wakati huo huo tuko tayari kuwa na tukio wakati wa vikao vya ngazi ya juu mwezi ujao wa Septemba ambapo nchi zilizo kwenye msitu huo na nchi zozoe zile zilizo tayari kusaidia zinaweza kujadiliana na kujitolea kulinda msitu huo muhimu,” amesema Katibu Mkuu.

Nchi za G7 ni Canada, Ufaransa, Ujeurmani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani.