Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya nchi 100 zimeahidi kusitisha na kubadilisha ukataji miti ifikapo 2030

Ukataji miti umewafurusha wanyama wengi kutoka katika makazi yao ya asili
Unsplash/Roya Ann Miller
Ukataji miti umewafurusha wanyama wengi kutoka katika makazi yao ya asili

Zaidi ya nchi 100 zimeahidi kusitisha na kubadilisha ukataji miti ifikapo 2030

Tabianchi na mazingira

Azimio la kihistoria la kuokoa na kurejesha misitu ya dunia katika ubora wake limetangazwa leo rasmi katika siku ya pili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi unaoshirikisha viongozi wa dunia au COP26.

Pamoja na viongozi makubaliano hayo yanaambatana na orodha ndefu ya ahadi kutoka kwa watendaji wa sekta za umma na binafsi kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kukabiliana na uharibifu wa viumbe hai na janga la njaa, na kulinda haki za watu wa jamii za asili.

Azimio hilo lililotiwa saini na viongozi linajikita na masuala ya misitu na matumizi ya ardhi likizitaka nchi kusitisha na kubadili mwelekeo wa ukataji miti katika muongo ujao kama sehemu ya mkakati wa mabilioni ya dola wa kupunguza gesi chafuzi ya viwandani  

"Leo itakuwa siku ya ukumbusho, tunaandaa mwongozo wa jinsi tunavyoweza kuhifadhi mapafu ya ulimwengu," amesema bwana Sandrine Dixson-Declève, ambaye akiwakaribisha washiriki wa tukio hilo kuu la viongozi  kwenye mkutano wa COP26.

Kauli za viongozi

Katika tangazo hilo la kihistoria viongozi wa kimataifa akiwemo Xi Jinping, Joe Biden na Jair Bolsonaro wametia saini azimio hilo la viongozi.

Waziri Mkuu wa Uingereza na mwenyeji mwenza wa COP26 Boris Johnson hakusita kusisitiza hitaji la dharura la kulinda misitu ya dunia hii, akisema “Mali hii ya asili ni muhimu sana kwa maisha yetu sasa n ahata siku zijazo. Kulinda misitu yetu sio tu muhimu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lkini pia kwa mustakbali bora wa dunia hii."

Wengine waliohudhuria ni pamoja na rais wa Marekani Joe Biden, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi, Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba na Rais wa Indonesia, Joko Widodo.

Kwa upande wake Rais wa Marekani Joe Biden ameangazia mchango wa Marekani kwa mahitaji ya dharura ya uhifadhi wa misitu, akitangaza kwamba kupitia mpango huo mpya, Marekani "itaisaidia dunia kutimiza lengo letu la pamoja la kukomesha upotevu wa misitu asilia na kurejesha angalau ekari milioni 200 za ziada za misitu na mifumo mingine ya ikolojia kufikia mwaka wa 2030.”

Akiwapongeza viongozi waliohudhuria mkutano huo Marais Biden, Tshishikedi na Bongo Ondimba kwa ahadi zao, Boris Johnson ameongeza kuwa anafurahi kutangaza katika mkutano huo kwamba "Duniani imekuja pamoja katika mkakati wa juhudi zao kwa kusanya angalau dola bilioni 1.5 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kusaidia kulinda nyanda za misitu na mifumo ya ikolojia yenye thamani kubwa ya Afrika ya Kati.”

Naye mwanzilishi wa Amazon na mwanahisani Jeff Bezos ametangaza ahadi ya dola bilioni mbili kama sehemu ya mpango huo, na kama sehemu ya ahadi yake ya dola bilioni kumi ya Bezos Earth Funds "kupambana na mabadiliko ya tabianchi  kuimarisha maliasili, kuendeleza haki ya mazingira na fursa za kiuchumi."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihitimisha akiwaasa viongozi kwamba “Kutia Saini azimio ni sehemu rahisi sana ya ahadi hiyo, lakini cha muhimu ni utekelezaji wake sasa kwa ajili ya wat una sayari hii.”

Takriban nusu ya eneo la ardhi oevu la Heilongjiang nchini China limepotea kutokana na ukataji miti na urejeshaji ardhi. (2018)
UNDP China
Takriban nusu ya eneo la ardhi oevu la Heilongjiang nchini China limepotea kutokana na ukataji miti na urejeshaji ardhi. (2018)

Nini kilichomo katika azimio hilo?

Katika tamko hilo, viongozi wanaahidi kuimarisha juhudi zao za pamoja za kuhifadhi misitu na mifumo mingine ya ikolojia ya nchi kavu na kuharakisha urejeshwaji wake, pamoja na kuwezesha sera endelevu za biashara na maendeleo, kimataifa na kitaifa.

Azimio pia linabainisha uwezeshaji wa jumuiya za wenyeji, ikiwa ni pamoja na watu wa kiasili, ambao mara nyingi husababisha kuathiriwa vibaya na unyonyaji na uharibifu wa misitu.
Azimio linalenga vilevile kutekeleza na kubuni upya sera na programu za kilimo ili kupunguza njaa na kunufaisha mazingira.

Fedha pia ni muhimu katika ahadi hiyo, ikiwa viongozi wameahidi kuwezesha upatanishi wa mtiririko wa fedha na malengo ya kimataifa ya kubadili upotevu na uharibifu wa misitu, huu ni wakati wa kuhakikisha sera za kuharakisha hatua za mpito kwa ajili ya uchumi wa kijani.

Katika muongo uliopita, takribani fedha mara 40 zaidi ziliingia katika matumizi mabaya ya ardhi badala ya ulinzi wa misitu, uhifadhi na kilimo endelevu.
Ahadi imetiwa saini pia na zaidi ya taasisi 30 za kifedha zinazohodhi zaidi ya dola trilioni 8.7 ya mali ya kimataifa chini ya usimamizi wake zinalenga kubadilisha hilo.  
Zinalenga pia kuondokana na pmipango inayowekeza katika minyororo ya ugavi wa bidhaa za kilimo zenye hatari kubwa ya ukataji miti na kuelekea katika uzalishaji endelevu.

Ahadi ya bonde la Congo

Tamko halikuishia hapo waandalizi wenza wa COP26 waliwasilisha ahadi ya Bonde la Congo, ambayo imetiwa saini na zaidi ya nchi 10, Mfuko wa kimataifa wa Bezos na Umoja wa Ulaya kukusanya dola bilioni 1.5 kulinda misitu, maeneo oevu na maeneo mengine muhimu yanayochangia hewa ukaa.

"Bonde la Congo ni moyo na mapafu ya bara la Afrika, hatuwezi kushinda vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa hatutalishikilia bonde hilo," amesema Rais wa Gabon, Ali Bongo Ondimba.
Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Uingereza, mpango huo pia ni sehemu ya ahadi mpya ya kimataifa ya ufadhili wa misitu ya zaidi ya dola bilioni 12.

"Ahadi kubwa zaidi za pamoja ya fedha za umma kwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika historia. Hebu tukomeshe maangamizi haya makubwa ya kimataifa kwa kutumia msumeno,” amesema.

Viongozi wa jamii za asili watoa kauli

Zaidi ya watu bilioni 1.6 duniani kote wanategemea misitu kwa ajili ya kuendesha maisha yao, na watu wa asili ndio walinzi wa angalau asilimia 36 ya misitu mikubwa duniani, isiyoharibika.

Ushahidi unaonyesha kuwa wananchi wa eneo hilo wanapowezeshwa kusimamia misitu hulindwa na kusimamiwa vyema.

Viongozi kadhaa wa jamii za asili kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameitikia azimio hilo kuhusu misitu Glasgow na ahadi ya kulinda ardhi wakati mkutano huo wa COP26.

"Iwapo asilimia 80 ya kile kinachopendekezwa kitaelekezwa katika kuunga mkono haki za ardhi na mapendekezo ya jamii za wenyeji na watu wa asili tutaona mabadiliko makubwa katika mwelekeo wa sasa unaoharibu maliasili zetu”, amesema Tuntiak Katak, makamu mratibu wa uratibu wa mashirika ya watu wa asili kutoka bonde la Amazoni (COICA).