Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yakaribisha dola milioni 250 kutoka Novartis kukabili magonjwa ya NTDs na malaria

Wadudu wanaopatikana Amerika kusini wanaoaminika kusababisha ugonjwa wa chagas.
CDC/David Snyder
Wadudu wanaopatikana Amerika kusini wanaoaminika kusababisha ugonjwa wa chagas.

WHO yakaribisha dola milioni 250 kutoka Novartis kukabili magonjwa ya NTDs na malaria

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataiofa duniani WHO leo limekaribisha tangazo kwamba shirika la dawa la Novartis litatoa dola za milioni 250 kwa ajili ya mapambano dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika (NTDs) na malaria.

Tangazo hilo limetolewa leo kwenye mkutano kuhusu malaria na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika NTDs unaofanyika Kigali Rwanda kandoni mwa mkutano wa 26 wa wakuu wa nchi na serikali za Jumuiya ya Madola (CHOGM). Azimio la Kigali, lililotangazwa katika mkutano huo, linalenga kuhamasisha dhamira ya kisiasa na ahadi zinazohitajika ili kufikia lengo la 3 la Umoja wa Mataifa la maendeleo endelevu ambalo ni "lengo la afya", linajumuisha NTDs, na kufikia malengo yaliyowekwa na WHO katika mkakati wa NTDs kwa mwaka 2021-2030. WHO inasema ahadi ya fedha iliyotangazwa na Novartis itasaidia kufadhili utafiti na maendeleo ya hali ya juu, na italenga hasa kutengeneza matibabu mapya, yenye ufanisi kwa kwa magonjwa ya NTDs ambayo ni pamoja na ugonjwa wa Chagas, homa ya denge, leishmaniasis ya visceral na malale pamoja na malaria. WHO pia inakaribisha ushirikiano uliojumuishwa katika uwekezaji, ambapo Novartis itashirikiana na The Wellcome Trust, mpango wa madawa kwa ajili ya magonjwa yaliyosahaulika na washirika wengine, kupambana na magonjwa ambayo yanaathiri maisha ya mamilioni ya watu katika baadhi ya jamii maskini zaidi duniani.