Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita, Machafuko na majanga mengine vyatawanya watoto milioni 36.5 mwaka 2021: UNICEF 

Watoto wa Darfur Kaskazini kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abo Shouk ambako UNAMID imekarabati darasa.
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Watoto wa Darfur Kaskazini kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abo Shouk ambako UNAMID imekarabati darasa.

Vita, Machafuko na majanga mengine vyatawanya watoto milioni 36.5 mwaka 2021: UNICEF 

Amani na Usalama

Vita, machafuko na mjanga mengine vimewaacha watoto milioni 36.5 wakitawanywa kutoka majumbani kwao hadi kufikia mwisho wa mwaka 2021 kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo linasema idadi hiyo ni kubwa kabisa kurekodiwa tangu vita ya pili ya dunia.

Takwimu hizo za UNICEF zinajumuisha watoto wakimbizi na waomba hifadhi milioni 13.7 na karibu watoto wengine zaidi ya milioni 22.8 ambao wametawanywa ndani ya nchi zao kutokana na vita na machafuko. 

Shirika hilo linasema takiwmu hizi mpya hazijumuishi watoto waliotawanywa na mabadiliko ya tabianchi au majanga mengine ya mazingira pamoja na wale waliotawanywa mwaka huu wa 2022  kutokana na vita ya Ukraine bali ni wale waliotokana na athari za moja kwa moja za vita vya muda mrefu kama vile vya Afghanistan, hali tete nchi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Yemen.

UNICEF imeonya kwamba hali ya watoto kutawanywa inaongezeka kwa kasi na mwaka jana pekee duniani kote kulikuwa na ongezeko la watoto milioni 2.2 waliotawanywa. 

Rania Dagash, naibu mkurugenzi wa UNICEF Kusini na Mashariki mwa Afrika (Kushoto) akikutana na mama wa watoto wmapacha wanaougua utapiamlo kwenye kituo cha afya cha Dollow Somalia
© UNICEF/Omid Fazel
Rania Dagash, naibu mkurugenzi wa UNICEF Kusini na Mashariki mwa Afrika (Kushoto) akikutana na mama wa watoto wmapacha wanaougua utapiamlo kwenye kituo cha afya cha Dollow Somalia

Hali halisi haiwezi kupuuzwa

Akisisitiza umuhimu wa kushughulikia hali hii mkurugenzi mtendani wa UNICEF Catherine Russell amesema “Hatuwezi kuupuuza ushahidi uliopo, idadi ya watoto wanaotawanywa na vita na migogoro inaongezeka haraka na vivyohivyo wajibu wetu wa kuwafikia watoto hawa. Natumai idadi hii ya kutisha itazifanya serikali kuchukua hatua ya kuzuia watoto kutawanywa na wanapotawanywa kuhakikisha wanakuwa na fursa ya kupata elimu, ulinzi na huduma zingine muhimu kwa ajili ya ustawi wao na maendeleo yao ya siku za usoni.” 

Flora Nducha
Vita, Machafuko na majanga mengine vyatawanya watoto milioni 36.5 mwaka 2021

Kwa upande wake Jean-Jacques Simon mkuu wa mawasiliano wa UNICEF nchini DRC moja ya nchi ambako watoto wengi wameathirika na vita vya muda mrefu anasema "Kwa UNICEF, wasiwasi ni kwamba watoto hawa wameacha nyumba zao, wameacha jamii zao na kwenda kila pembe, kwa hiyo hofu yetu ni ulinzi wao, ukizingatia ukweli kwamba mara nyingi hawana maji na hawana dawa. Kwa siku chache zijazo, au wiki chache zijazo, tunachohofia ni kwamba hawatakuwa na mazingira ambayo kuna shule, ambapo kuna mwavuli wa kinga na ndio maana tuko hapa kushuhudia hali hii inayotia wasiwasi. " 

Mambo sita ya kuzingatia kulinda watoto

Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

Twakimu hizo mpya pia zimetaja majanga mengine ya asili kama ukame kwenye Pembe ya Afrika na Sahel, mafuriko Bangladesh, India na Afrika Kusini kwamba yameongeza zahma ya kutawanya watoto wengine wapya milioni 7.3 mwaka 2021. 

Kwa mantiki hiyo UNICEF imetoa wito kwa nchi wanachama kuchukua hatua ili kufia mambo sita yatakayohakikisha haki na fursa kwa watoto wote wakimbizi, wahamiaji na waliotawanywa na kulinda haki za watoto ikiwa ni pamoja na mosi kutambua kwamba watoto wakimbizi, wahamiaji na waliotawanywa la kwanza kabisa ni watoto na hivyo wanastahili haki ya kulindwa, kuendelezwa na kushirikishwa.  

Pili kuongeza hatua za pamoja kuhakikisha wanapata fursa za huduma muhimu ikiwemo za afya na elimu, tatu kuwalinda watoto hao wakimbizi, wahamiaji na waliotawanywa dhidi ya ubaguzi na chuki dhidi ya wageni. 

Nne kutokomeza hulka zinazoathiri watoto mipakani pamoja na kuacha kuweka watoto mahabusu. 

Tano kuwawezesha vijana wakimbizi, wahamiaji na waliotawanywa ili kuweza kuonyesha vipaji vyao na kufikia uwezo wao kamili na sita kuhakikisha haki zao zote zinadumishwa.