Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wavenezuela bado wanaendelea kufungasha virago na kuingia Brazil wakiwemo watoto:UNICEF

Mamia ya wavenezuela wakiwa mpakani mwa Colombia wakisubiri kuvuka.
UNICEF/Santiago Arcos
Mamia ya wavenezuela wakiwa mpakani mwa Colombia wakisubiri kuvuka.

Wavenezuela bado wanaendelea kufungasha virago na kuingia Brazil wakiwemo watoto:UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema maelfu ya watoto bado wanaendelea kuwa waathirika wa hali mbaya nchini Venezuela na kulazimika na familia zao kufungasha virago na kuingia nchi jirani ya Brazil.

Katika ziara ya siku nne iliyofanywa na balozi mwema wa shirika la UNICEF Liam Neeson kwenmy mji wa Brazil ulioko mpakani na Venezuela ameshuhudia hali halisi baada ya kukutana na Watoto na familia zao lakini pia jamii zinazowahifadhi.

Katika ziara hiyo ya siku tatu iliyomalizika mwishoni mwa wiki Neeson amete,mbelea Rondon 3, moja ya makazi makubwa zaidi yanayohifadhi wahamiaji wa Venezuela nchini Brazili. Watu Zaidi ya 1000 wakiwemo Watoto 550 wanaishi katika makazi haya hivi sasa.

Kama hatua za kukabiliaka na wimbi kubwa la wahamiaji wa Venezuela kuingia Brazil , UNICEF na washirika wake wamechukua hatua mbalimbali hasa katika masuala ya elimu na ulinzi kwa Watoto, afya na lishe, pamoja na masuala ya maji na usafi.

Moja ya vitu walivyofanya ni kufungua mahali pa kukutanisha watoto kituo kiitwacho Super Panas ambacho kinatoa huduma za elimu, michezo na msaada wa kisaikolojia ili kuandaa watotona vijana barubaru kujumika katika shule za kawaida au kuwasaidia ambao tayari wameingia shuleni.

Balozi mwema alishiriki katika shughuli mbalimbali na Watoto hao na vijana barubaru na pia kuhudhuria huduma za afya za upimaji kwa ajili ya Watoto hao wahamiaji.

Kwa kushirikiana na mamlaka na mashirika ya Umoja wa Mataifa Ecuador, Peru, Brazil, Colombia, Guyana na Trinidad na Tobago, UNICEF pia inaongeza hatua zake katika maeneo ya mijini na kusaidia kujumuishwaji wa Watoto kutoka Venezuela katika jamii zinazowahifadhi.

Nchi za Amerika Kusini na Caribbea tayari zinahifadhi wahamiaji na wakimbizi milioni 3.9 kutoka Venezuela katika moja ya kinachojulikana kama wimbi kubwa zaidi la wahamiaji.

Na idadi ya familia zinazoondoka Venezuela inazidi kuongezeka . Mwaka huu watoto zaidi ya milioni 1.9 wakiwemo wahamiaji toka Venezuela na jamii zinazowahifadhi wanatarajiwa kuhitaji msaada.

Na hadi kufikia Desemba 2019 ni asilimia 41 pekee ya dola milioni 69.5 zizilizohitajika mwaka jana ndio zimepatikana na mwaka huu UNICEF inahitaji dola milioni 64 ili kukidhi mahitaji ya takriban watoto 633,000 walioathirika na uhamiaji toka Venezuela, wakiwemo ambao wako safarini na jamii zinazowahifadhi katika nchi sita za Amerika ya Kusini ikiwemo Brazil.