Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 30 waliotawanywa na vita wanahitaji kulindwa, na pia suluhu ya kudumu:UNICEF

Watoto hawa wakiwa kwenye makazi ya wahamiaji huko Niamey nchini Niger, ambako watu wengi huishi baada ya kufukuzwa kutoka Algeria
IOM Niger
Watoto hawa wakiwa kwenye makazi ya wahamiaji huko Niamey nchini Niger, ambako watu wengi huishi baada ya kufukuzwa kutoka Algeria

Watoto milioni 30 waliotawanywa na vita wanahitaji kulindwa, na pia suluhu ya kudumu:UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani watoto milioni 30 waliotawanywa na vita duniani wanahitaji ulinzi sasa na suluhu endelevu na ya kudumu kwa ajili ya mustakbali wao.

Wito huo umetolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika kuelekea siku ya wakimbizi duniani ambayo kila mwaka huwa Juni 20, wakati wauzinduzi wa mkakati wa kushirikisha wapenzi wa kandanda ili kuunga mkono watoto wakimbizi na wahamiaji i ujulikanao kama “Nini kinachotusisimua, nini kinachotounganisha”

UNICEF inasema idadi ya watoto milioni 30 ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote tangu vita vya pili vya dunia, na kuonya kwamba watoto hawa ambao hawajiwezi wanahitaji fursa ya kulindwa na huduma muhimu ili kuwaweka salama sasa lakini pia kuhakikisha usalama wao kwa siku za usoni.

Nini kinachotusisimua, nini kinachotuunganisha

Shirika hilo pia limewataka viongozi wa dunia kuongeza mara mbili juhudi zao za kuhakikisha haki, usalama na mustakbali wa watoto wasiojiweza ambao wengi wao bado wametawanywa na vita, machafuko na hali tete ya kisiasa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa masuala ya dharura wa UNICEF Manuel Fontaine, katika siku ya wakimbizi duniani ni muhimu kukumbuka vitisho na changamoto wanazopitia watoto wanaokimbia makwao na hasa kuondoa vikwazo vinavyofuta matumaini ya mustakhbali wao.

Wakati huu ambapo kandanda imewaleta mashabiki pamoja kutoka kote duniani kwenye kombe la dunia, UNICEF na mdau 180LA, wanapigia chepuo mkakati wa “Nini kinachotusisimua, nini kinachotuunganisha” kwa imani kwamba endapo mapenzi ya michezo kama soka yanaweza kuvuka mipaka basi vivyo hivyo kuwaunga mkono watoto wakimbizi na wahamiaji inawezekana kuvuka mipaka.