Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau wauvuvi waishukuru FAO kwa Mradi wa FISH4ACP

Kikosi kazi cha mradi wa FISH4ACP unaoendeshwa na FAO nchini Tanzania
UN News
Kikosi kazi cha mradi wa FISH4ACP unaoendeshwa na FAO nchini Tanzania

Wadau wauvuvi waishukuru FAO kwa Mradi wa FISH4ACP

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO linaendelea na jitihada za kuhakikisha tija inapatikana katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao yatokanayo na uvuvi nchini Tanzania kupitia mradi wake wa FISH4ACP unaotekelezwa nchini humo katika mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi.

Kutokana na sekta ya uvuvi kukabiliwa na changamoto mbalimbali, FAO imeona kuna haja ya kufanya  jitihada za kuhakikisha tija katika mnyororo mzima wa  thamani wa mazao yatokanayo na uvuvi na ndio msingi wa kuwa na mradi wa namna hii  ambao unatekelezwa katika nchi 12 barani afrika, tanzania nayo ikiwemo.

Betina Tito mchakataji katika mwalo wa kibirizi mkoani kigoma anaeleza mabadiliko yaliyopo tangu kuanza utekelezaji wa mradi. “Mradi huu wa FSH4ACP kwangu mimi naweza kusema umetusaidia sisi wachakataji kwa sababu tuna changamoto nyingi lakini tangu mradi umeanza zimepungua maana tumeelimika, wanawake tunachangamana na wanaume. Kabla ya mradi mwanamke alikuwa hawezi kupata mzigo mpaka achukue atoe vijipesa kidogo sasa hivi hali haipo hivyo, walitufundishwa tusiwe waoga na tujitahidi kuunda vikundi.”

Mwingine niliyezungumza naye ni Francis John ambaye ni Mwenyekiti wa vyama vya ushirika wa wavuvi mkoa wa Kigoma ameipongeza FAO kwa mafanikio yaliyopatikana, anaeleza kilio chao kikubwa kinachowakabili kwa sasa.“Unajua hata mtu angelikupa pesa halafu asikwambie ufanye kazi gani haziwezi kukusaidia, lakini kwanza akupe elimu na elimu ambayo tunayo ni ya kulinda mazingira na kujua kwamba unaponunua zile dagaa, ukazichakata unatakiwa uziuze kwa njia gani, na mahali unapozichakata pawe salama ili unaowauzia uwauzie kitu ambacho ni safi.” 

Na baadaya kupata elimu na kujihakikishia mnyororo wa thamani utakuwa na manufaa kwao Francis ametoa ombi kwa serikali “Tunatamani kwamba serikali itusaidie na mitaji pia ituunganishe na mabenki ili tupate mitaji ya kutosha kwa sababu dagaa au samaki zinaweza kupatikana ila mitaji ikawa Midogo,”

Hashim Muumin  Mratibu wa Mradi wa FISH4ACP mkoani Kigoma akizungumza katika kikao cha kikosi kazi
UN News
Hashim Muumin Mratibu wa Mradi wa FISH4ACP mkoani Kigoma akizungumza katika kikao cha kikosi kazi

Kwa upande wake Hashim Muumin ambaye ni Mratibu wa mradi wa FISH4ACP kutoka FAO anasema licha ya kuwajengea uwezo wadau wa uvuvi lakini mradi unalenga kudhibiti upotevu wa mazao ya uvuvi.

“Tunawapa mafunzo  wavuvi kuhakikisha mazao yanafika mwaloni yakiwa  hajaharibika lengo ni kupunguza upotevu wa mazao kwasababu kutokana na utafiti tuliofanya, ni asilimia 16 ndio kuna upotevu wa mazao na kiwango hichi kinazidi kipindi cha msimu wa mvua kila hatua  kuanzia kwa mvuvi, mchakataji, msafirishaji na muuzaji, kwahiyo tumeweka hiyo mikakati kukabili upotevu wa mazao katika maeneo hayo,”amebainisha Mratibu huyo.

Miradi ya FAO inahusisha pande zote yaani wananchi na serikali. Masui Munda  ni Mteknolojia mwandamizi katika wizara ya mifugo na uvuvi na pia ni afisa dawati wa mradi huo anaeleza fursa zinazotokana na mradi  kwa mujibu wa wizara yenye dhamana.

“Mradi kwa upande wa Serikali imekuja na dhana ile ambayo wizara inaenda nayo ya kuhakikisha kwamba mazao ya uvuvi hususani dagaa yanafanya vizuri kuinua kipato cha wananchi na kuchangia pato la Taifa kwa upande wa wizara sasa hivi dagaa ni zao la kimkakati kwahiyo wizraa inatuamia fursa kuhakikish amnyororo wa thamani wa mazao haya unakuzwa,”ameeleza Masui.

Masui anahitimisha kwa kubainisha uboreshwaji wa nyanja ya vifungashio vya mazao ya uvuvi. “Changamoto ya vifungashio, katika kikao hiki limekuwa ni eneo ambalo tumeliangalia kupitia mradi huu ni mradi amabao chimbuko lake ni serikalini sasa suala la mikopo ni sehemu mojawapo ambayo mradi huu unaliangalia tumeweka mazingira ya kuwawezesha wachakataji, wavuvi, na wafanyabiashara,” amehitimisha Mteknolojia huyo.