Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zatakiwa kuimarisha huduma za afya ya akili wakati zikikabiliana na mabadiliko ya tabianchi

UNICEF inatoa huduma ya afya ya akili wa wanawake nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Michael Duff
UNICEF inatoa huduma ya afya ya akili wa wanawake nchini Sierra Leone.

Nchi zatakiwa kuimarisha huduma za afya ya akili wakati zikikabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabianchi yanahatarisha sana afya ya akili na ustawi ndio maana hii leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limetoa muhtasari wa sera inayo himiza nchi kujumuisha usaidizi wa afya ya akili katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Sera hiyo mpya imezinduliwa leo na WHO kwenye mkutano wa Stockholm+50 nchini Sweden baada ya utafiti kuonesha athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku, huku kukiwa na usaidizi mdogo sana wa kujitolea wa afya ya akili unaopatikana kwa watu na jamii zinazohusika na hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi na pia hatari za muda mrefu.

Utafiti uliofanywa na WHO mwaka jana 2021 katika nchi 95 uligundua kuwa ni nchi 9 tu hadi sasa ndizo zimejumuisha msaada wa afya ya akili na kisaikolojia katika mipango yao ya kitaifa ya afya na mabadiliko ya tabianchi. 

Matokeo haya yanalingana na ripoti ya hivi karibuni ya jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC iliyofichua kuwa mabadiliko ya tabianchi yanayoongezeka kwa kasi yanaleta tishio linalokua kwa afya ya akili na ustawi wa kisaikolojia.

Mkurugenzi wa WHO, Idara ya afya ya akili na matumizi mabaya ya madawa Dévora Kestel, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hali ambayo tayari ni changamoto kwa afya ya akili na huduma za afya ya akili ulimwenguni.

“Kuna takriban watu bilioni 1 wanaoishi na hali ya afya ya akili, lakini katika nchi za kipato cha chini na cha kati, watu watatu kati ya wanne hawapati huduma zinazohitajika”. Kwa kuongeza msaada wa afya ya akili na kisaikolojia ndani ya kupunguza hatari ya maafa na hatua za hali ya hewa, nchi zinaweza kufanya zaidi kusaidia kuwalinda walio hatarini zaidi.”

Sera hiyo mpya imependekeza masuala matano muhimu kwa serikali ya kushughulikia ambayo ni

• Kuunganisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi na programu za afya ya akili

• Kuunganisha usaidizi wa afya ya akili na hatua za kupamabana na mabadiliko ya tabianchi

• Kuweka ahadi za kimataifa

• Kubuni mbinu za kijamii zitakazopunguza udhaifu, na

• Kuziba pengo kubwa la ufadhili lililopo kwa ajili ya afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia na kijamii

WHO inasema nchi ya Ufilipino ni moja ya mfano mzuri wa kujumuisha mabadiliko ya tabianchi na afya ya akili ambapo baada ya kutokea kimbunga Haiyan mwaka 2013, imejenga upya na kuboresha huduma zake za afya ya akili na mradi huo wa kitaifa umesaidia kupunguza hatari ya maafa.

Dk Diarmid Campbell-Lendrum, ambaye ni kiongozi mkuu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi wa WHO na mwandishi mkuu wa  IPCC amesema “Nchi wanachama wa WHO zimeweka wazi kuwa afya ya akili ni kipaumbele kwao. Tunafanya kazi kwa karibu na nchi ili kulinda afya ya watu ya kimwili na kiakili kutokana na matishio ya hali ya hewa”.