Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya COVID-19 Afrika kupungua kwa takriban asilimia 94: WHO 

Mwanamke akionesha kadi ya chanjo ya COVID-19 akiwa na jamaa zake Kano, Nigeria.
© UNICEF
Mwanamke akionesha kadi ya chanjo ya COVID-19 akiwa na jamaa zake Kano, Nigeria.

Vifo vya COVID-19 Afrika kupungua kwa takriban asilimia 94: WHO 

Afya

Vifo vya COVID-19 katika ukanda wa Afrika vinatarajiwa kupungua kwa karibu asilimia 94 mwaka huu 2022 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo janga hilo lilikuwa katika kilele cha athari zale, kwa mujibu wa tathimini ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO iliyotolewa leo. 

Shirika hilo linasema hilo ni punguzo kubwa kutoka takriban vifo 970 kila siku mwaka jana hadi vifo karibu 60 kwa siku ifikapo mwisho wa mwaka huu. 

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “Idadi ndogo ya vifo inayotarajiwa mwaka huu ni mafanikio makubwa katika Ukanda wa Afrika na ushuhuda wa jitihada zilizofanywa na nchi za bara hilo na wadau mbalimbali. Hata hivyo kazi bado haijamalizika, kila muda tunapobweteka COVID-19 inashambulia tena.” 

Mwanamume apokea chanjo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
© UNICEF/Jean-Claude Wenga
Mwanamume apokea chanjo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

 

Kuendelea kukaa chonjo  

Ropoti hiyo ya tathimini liyochapishwa wiki hii kwenye jarida la kitabibu  la Uingereza Lancet imekuja wakati idadi ya wagonjwa inakadiriwa kupungua kwa zaidi ya robo mwaka huu. Jumla ya vifo 350,000 vinakadiriwa kutokea mwaka jana. 

Na sasa tathimini hiyo inakadiria kwamba kutakuwa na vifo 23,000 vinavyotarajiwa ifikapo mwisho wa mwaka huu endapo mwenendo wa sasa hautobadilika. 

WHO imesema lakini, lahaja ambayo ni asilimia 200 mbaya zaidi, inaweza kusababisha ongezeko la vifo hadi kufikia zaidi ya 70,000. 

"Tishio la lahaja mpya linasalia kuwa halisi, na tunahitaji kuwa tayari kukabiliana na hatari hii inayoendelea," ameonya Dkt. Moeti. 

Visa ambavyo havijaripotiwa 

Matokeo ya utafiti huo yanadokeza kwamba ni kisa kimoja tu kati ya visa 71 vya COVID-19 barani Afrika ndio ambayvo vimerekodiwa na inakadiriwa maambukizo 166. 2 milioni mwaka huu ikilinganishwa na makadirio ya milioni 227.5 yaliyotokea mwaka jana 2021. 

Kwa mujibu wa WHO “Kupungua kwa idadi ya wagonjwa na na vifo mwaka 2022 kunatokana na kuongezeka kwa chanjo, uboreshaji wa hatua za kukabiliana na janga hilo na kinga ya asili dhidi ya maambukizo ya hapo awali ambayo, ingawa hayazuii maambukizo tena, yanazuia hali ya wagonjwa kuwa mahtuti inayoweza kusababisha kifo. 

Mwaka wa vifo vingi 

Uchambuzi huo unakadiria kuwa COVID-19 ilikuwa sababu ya saba kuu ya vifo barani Afrika mwaka jana, baada ya malaria. 

Ongezeko kubwa la vifo na wagonjwa mwaka jana lilitokana na lahaja ya Delta iliyoambukiza kwa kasi zaidi na iliyokuwa kali zaidi. 

Kuongeza huduma 

 

"Tumejifunza mambo mengi kuhusu jinsi ya kuwa hatua moja mbele ya virusi," amesema Dk. Moeti. 

Kadiri janga hili linavyoendelea, WHO inasisitiza kwamba ni muhimu kuimarisha huduma za afya za kina, ikiwa ni pamoja na hatua za kuzuia, matibabu na chanjo kwa watu walio katika hatari zaidi. 

Ufuatiliaji wa kulenga makundi fulani pia utakuwa muhimu ili kufuatilia kulazwa hospitalini, mzigo wa magonjwa na kuibuka kwa lahaja mpya. 

Bi Moeti ameongeza kuwa "Sasa ni wakati wa kuboresha hatua zetu na kutambua idadi ya watu walio katika hatari kubwa ya COVID-19. Ni lazima nchi ziongeze juhudi za kuchukua hatua za kulenga ambazo huwapa watu walio hatarini zaidi huduma za afya wanazohitaji, ikijumuisha chanjo ya COVID-19 na matibabu madhubuti." 

Maelezo ya vifo 

Vifo vya COVID-19 havilingani katika eneo lote la Afrika. 

Nchi za kipato cha juu au za kipato cha kati karibu na cha juu na zile za Jumuiya ya maendeleo ya Afrika Kusini (SADC) zina karibu mara mbili ya viwango vya vifo kuliko nchi za kipato cha chini na cha kati katika kanda zingine za kiuchumi za Afrika. 

Uchanganuzi unaonyesha kuwa tofauti ya idadi ya vifo ilichangiwa na sababu za kibaolojia na za kinga ya mwili haswa kutokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, ugonjwa sugu wa mapafu, VVU, na unene wa kupindukia ambayo huongeza ukali na hatari ya vifo kwa wagonjwa wa COVID-19. 

"Viwango tofauti vya vifo kati ya nchi katika kanda vinasisitiza haja ya hatua zilizowekwa," amesema Dkt. Moeti. Na kuongeza kuwa "Kadri gonjwa linavyoendelea, kilicho wazi ni kwamba vitendo vyetu vinahitaji kuendana na kile kinachobaki kuwa hali inayobadilika na ngumu". 

Baada ya mlipuko wa mnyumbuliko wa virusi vya Corona, Omicron, WHO ilitangaza kuiunga mkono Afrika huku ikishauri kutofungwa kwa mipaka.
WHO/Africa
Baada ya mlipuko wa mnyumbuliko wa virusi vya Corona, Omicron, WHO ilitangaza kuiunga mkono Afrika huku ikishauri kutofungwa kwa mipaka.

 

Omicron inatoa kinga ndogo dhidi ya kuambukizwa tena 

Takwimu mpya kuhusu janga hili la COVID-19 kote duniani zilizotolewa leo na WHO zinaeleza kwamba watu ambao wameambukizwa lahaja ya Omicron kinga dhidi ya kutoambukizwa tena COVID-19 ni ndogo.  

Ushahidi wa hivi karibuni  wa WHO “pia unaonyesha kuwa kinga dhidi ya ugonjwa huo mbaya wa COVID-19 ni thabiti zaidi miongoni mwa wale ambao wameambukizwa ugonjwa huo na pia wakapata chanjo kuliko ilivyo kwa watu ambao ama wameambukizwa tu, au walipata chanjo tu.” 

Kipaumbele cha mashirika ya afya ya kitaifa kinapaswa kuwa chanjo ya watu wazima wote, ikilenga wafanyikazi wa afya, watu walio na kinga duni na wazee, limesema shirika la WHO.