Skip to main content

Nchi 23 katika kanda zote za WHO tayari zimeripoti virusi vya Omicron

Mwanamke mkimbizi akipata chanjo ya kwanza ya COVID-19 ya Sinopharm
UNHCR Indonesia
Mwanamke mkimbizi akipata chanjo ya kwanza ya COVID-19 ya Sinopharm

Nchi 23 katika kanda zote za WHO tayari zimeripoti virusi vya Omicron

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema leo nchi wanachama wameamua kuanza mchakato wa kuandaa na kujadiliana kuhusu mkataba mpya , makubaliano au chombo kingine cha kimataifa kwa ajili ya kuzuia mlipuko wa magonjwa, kujiandaa na kukabilisna nao. 

Akizungumza katika mkutano wa kila wiki wa kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa COVID-19, mjini Geneva Uswisi hii leo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema

“Dharura ya kuibuka kwa kirusi kipya cha Omicron kumeamsha umakini wa kimataifa. Angalau nchi 23 kutoka kanda zote sita za WHO sasa zimeripoti kesi za Omicron, na tunatarajia idadi hiyo kuongezeka.” 

Ameongeza kuwa kufuatia dharura hiyo “Tunatoa wito kwa nchi zote kuchukua hatua za busara, zenye usawa za kupunguza hatari, kwa kuzingatia kanuni za afya za kimataifa. Hatupaswi kusahau kwamba tayari tunakabiliana na aina nyingine na ambayo ni ya hatari na inayosambaa ya Delta, ambayo kwa sasa inaongoza kwa iadadi ya wagonjwa wapya wote wa COVID-19 duniani.”

Amesema duniani kote kuna mchanganyiko wa sumu ya kiwango cha chini cha chanjo na kiwango cha chini cha upimaji  ambavyo ni vichocheo vya kuzaliana na kusambaa kwa virusi. 

Kwa mantiki hiyo Dkt. Tedros amekumbusha kwamba “Tunapoadhimisha siku ya ukimwi duniani, tunakumbushwa kwamba zaidi ya miaka 40 ya janga la UKIMWI duniani, bado hatuna chanjo na tiba ya ugonjwa huu. Miaka miwili katika janga la COVID-19, hatuna chanjo moja lakini tunazo nyingi, na zana zingine nyingi zinazofaa.” 

Mwanasayansi akipima sampuli za COVID-19 katika maabara nchini Sierra Leone.
WHO
Mwanasayansi akipima sampuli za COVID-19 katika maabara nchini Sierra Leone.

Mkuu huyo wa WHO ameitaka kila nchi kuwa makini na virusi vipya vya Omicron “WHO inachukulia maendeleo haya kwa umakini mkubwa, na vivyo hivyo kwa kila nchi. Lakini isitushangaze hivi ndivyo virusi hufanya. Tunatoa wito kwa nchi zote kuchukua hatua za tahadhari kama mvile kukagua abiria kabla ya kusafiri na/au wanapowasili, au kutumia karantini kwa wasafiri wa kimataifa. Marufuku ya kusafiri kwa wote haitazuia kuenea kimataifa kwa irusi vya Omicron, na inaweka mzigo mzito kwa maisha na riziki za watu.”

WHO inaendelea kutoa wito kwa nchi zote kuboresha afya ya umma na hatua za kijamii, na kuhakikisha kuwa watu walio katika hatari kubwa na walio hatarini zaidi katika nchi zote wanapata chanjo kamili mara moja. 

“Tunahitaji kutumia zana ambazo tayari tunazo ili kuzuia maambukizi na kuokoa maisha kutokana na virusi vya Delta. Na tukifanya hivyo, tutazuia pia maambukizi na kuokoa maisha kutoka kwa Omicron. Lakini ikiwa nchi na watu binafsi hawatafanya kile wanachohitaji kufanya ili kukomesha maambukizi ya Delta, hawatamzuia Omicron pia.” Amesisitiza Dkt. Tedros 

Ameongeza kuwa “Virusi hivi vimeonyesha kuwa havitatoweka tu. Ni maisha mangapi zaidi na riziki ngapi zaidi ambazo zitachukuliwa  na virusi hivi, hiyo ni juu yetu. Kukomesha janga hili si jambo la kubahatisha, ni suala la kuchagua.”