Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha maambukizi ya COVID-19 Afrika cha chini zaidi tangu April 2020 

Mhudumu wa afya akiwa ameshika vifaa tiba Toro, Bauchi, Nigeria.
© UNICEF/Andrew Esiebo
Mhudumu wa afya akiwa ameshika vifaa tiba Toro, Bauchi, Nigeria.

Kiwango cha maambukizi ya COVID-19 Afrika cha chini zaidi tangu April 2020 

Afya

Maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 barani Afrika yamekuwa ni ya chini zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuripotiwa kwa mara ya kwanza kwa mlipuko huo mwezi Aprili mwaka 2020, ambapo idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki 16 zilizopita imepungua sambamba na idadi ya vifo katika wiki 8 zilizopita. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, Kanda ya Afrika limesema hayo hii leo kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Brazaville, Congo. 

Maambukizi, kwa kiasi kikubwa yakitokana na wimbi la nne la mnyumbuliko wa virusi vya Omnicron, yamepungua kutoka wagonjwa 308,000 kwa wiki mwanzoni mwa mwaka huu hadi chini ya wagonjwa 20,000 katika wiki inayoitishia tarehe 1 mwezi huu wa Aprili,” imesema taarifa hiyo. 

Katika wiki moja iliyopita, takribain kulikuwa na wagonjwa 18,000 na vifo 239, idadi ambayo imepungua kwa asilimia 29 na 37 mtawalia, ikilinganishwa na wiki iliyotangulia. 

“Idadi hii ni kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa barani Afrika tangu mwezi Aprili mwaka 2022, janga la COVID-19 lilipokuwa katika hatua za awali, Afrika" imesema taarifa hiyo. 

Kuwepo kwa kipindi cha muda mrefu cha idadi ndogo ya maambukizi na vifo barani Afrika kutokana na COVID-19 ilishuhudiwa kati ya Agosti 1 na Oktoba 10 mwaka 2021. 

WHO inasema kwa sasa hakuna nchi Afrika inayoshuhudia ongezeko la COVID-19. 

Hata hivyo Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti anasema “licha ya kupungua kwa maambukizi, ni vyema nchi zikaendelea kuwa makini na kuzingatia mikakati ya kujikinga ikiwemo uchunguzi na ufuatiliaji sambamba na kusisitiza upimaji.” 

Amesema kwa kuwa virusi hivyo bado vipo, kuna hatari ya kuibuka kwa mnyumbuliko mpya na kwamba hatua za kudhibiti janga hilo la COVID-19 ni vema kuzingatiwa ili kudhibiti mlipuko. 

Hofu ni kwamba msimu wa baridi kali unakaribia ukanda wa kusini mwezi Juni hadi Agosti, “hivyo kuna hatari ya maambukizi mapya kwa kuwa katika bara la Afrika, viwango vya chini ya joto vimechochea maambukizi kwani watu wanasalia ndani muda mrefu ambako hakuna mzunguko mzuri wa hewa." 

Kutokana na hali ya sasa ya maambukizi, WHO inasihi nchi kujipima zenyewe juu ya hatari na faida za kulegeza masharti ya COVID-19 kwa kuzingatia uwezo wa mifumo yao ya afya, kinga waliyo nayo wananchi dhidi ya COVID-19 na vipaumbele vya kiuchumi na kijamii vya kitaifa. 

“Kuweko na utaratibu ambao unaweza kurejesha haraka mifumo ya usimamizi na udhiibti wa COVID-19, iwapo mlipuko utaibuka tena,” imetamatisha taarifa hiyo ya WHO.