Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani haipatikani kwa mtutu wa bunduki bali kwa njia ya upendo:Walinda amani DRC 

Walinda amani wa MONUSCO wakifanya doria eneo la Beni nchini DRC.
UN Photo/Sylvain Liechti
Walinda amani wa MONUSCO wakifanya doria eneo la Beni nchini DRC.

Amani haipatikani kwa mtutu wa bunduki bali kwa njia ya upendo:Walinda amani DRC 

Amani na Usalama

Kila mwaka tarehe 29, mwezi wa Mei Umoja wa mataifa huadhimisha siku ya walinda amani duniani, na leo hapa kwenye makao makuu imefanyika hafla maalum ya kuadhimisha siku hiyo muhimu ya kukumbuka mchango wa walinda amani duniani, ambao ni wake kwa waume wanaohudumu kama wanajeshi, polisi ama raia kwenye majukumu ya ulinzi wa amani. 

Aidha, siku hii ni muhimu pia katika kuenzi mchango wa walinda amani waliopoteza maisha wakipigania amani katika mataifa mbalimbali duniani. 

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazochangia walinda amani katika maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na vita ikiwemo Lebanon, Jamuhuri ya Afrika ya Kati CAR, Msumbiji pamoja na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Afisa Habari wa kikosi cha 9 cha Tanzania nchini DRC au TANZBAT 9 Kapteni Denisia Lihaya amezungumza na baadhi ya walinda amani wa kikosi hicho kuhusu majukumu yao na wanavyoshirikiana na wadau wengine kutimiza wajibu wao.  

Koplo Joyce Seti Sanga ni fundi magari katika kikosi cha TANZBAT 9
MONUSCO/Captain Denisia Lihaya
Koplo Joyce Seti Sanga ni fundi magari katika kikosi cha TANZBAT 9

Kiini cha amani ni upendo 

Koplo Joyce Seti Sanga ni fundi magari katika kikosi cha TANZBAT 9 anasema majukumu yake ni kuhakikisha magari yote yanakaguliwa kabla ya kutoka kituoni kwenda kwenye shughuli mbalimbali na kuhakikisha yako salama kutekeleza majukumu na zoezi hilo hufanyika pia baada ya magari kurejea kituoni mwisho wa siku. 

Anasema kazi hiyo hafanyi peke yake “Tunashirikiana na nchi mbalimbali zilizoko hapa Congo kwa ajili ya ulinzi wa amani ambazo ni Afrika Kusini, Malawi na wacongo wenyewe”. 

Akaenda mbali zaidi katika kuelekea siku ya walinda amani na kutoa ujumbe kwa raia wa Congo wanaowahudumia akisema “Upendo ni kitu kidogo sana lakini kina maana wakiamini katika upendo machafuko yataisha, hivyo nawasihi sana waishi katika upendo. Tukiishi ndani ya upendo dunia nzima itakuwa na amani, hivyo nawaomba waamini kwamba ndani ya upendo kuna amani.” 

Luteni Denis Njaku kamanda wa platuni kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
MONUSCO/Captain Denisia Lihaya
Luteni Denis Njaku kamanda wa platuni kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.

MONUSCO ipo hapa kwa ajili yenu Wacongo 

Akiunga mkono kudumisha upendo Luteni Denis Njaku kamanda wa platuni anasema majukumu yake makubwa ni kuhakikisha ulinzi na usalama wa rai awa DRC. 

Mbali ya kukabiliana na magaidi au waasi majukumu yake pia akishirikiana na wengine ni kuunga mkono shughuli za jamii ambazo zinahitaji ulinzi wa walinda amani. Na katika kufanikisha majukumu hayo Njaku anasema “Tunashirikiana na vikosi mbalimbali vya kutoka mataifa mengine kama vile Afrika Kusini, Malawi Kenya, na kikosi cha serikali ya Congo na kikosi cha polisi cha DRC katika operesheni mbalimbali ikiwemo doria.” 

Kwa raia wa Congo Luteni Njaku amewakumbusha kwamba walinda amani wako hapo kwa ajili yao. 

“Rai yangu kwa wananchi wa Congo ni kwamba MONUSCO iko hapa kwa ajili yao, wasisite kutoa changamoto ambazo wanakutana nazo sio tu kwa waasi bali hata za kijamii. Tuko hapa kwa ajili yao, tuko hapa kuwasia wao na tupo hapa kufanya Congo iwe na amani kama kaulimbiu inavyosema watu, amani na hatua zilizopigwa.” 

Luteni Njaku akawageukia walinda amani wenzie na kuwaambia “Walinzi wa amani dunia nzima tutende haki. Hakuna haja ya kurudisha risasi kwa jiwe.” 

Pili Ali Silima stafu sajenti ambaye ni karani mkuu wa TANZBAT 9 akisimamia makarani wengine wa kikosi chake.
MONUSCO/Kapteni Denisia Lihaya
Pili Ali Silima stafu sajenti ambaye ni karani mkuu wa TANZBAT 9 akisimamia makarani wengine wa kikosi chake.

Chonde chonde wapiganaji wekeni salaha chini 

Naye Pili Ali Silima stafu sajenti ambaye ni karani mkuu wa TANZBAT 9 akisimamia makarani wengine wa kikosi chake, lakini pia kazi zote zinazoletwa kukota vikosi vingine vya TANZBAT. 

Kazi yake inampa fursa ya kushirikiana na vikosi vya mataifa mengine hasa wakati wa kufanya maombi ya vifaa, au maombi ya askari wanaotakiwa kujumuika kwenda kwenye operesheni za kutuliza machafuko katika sehemu mbalimbali za DRC. 

Stafu sajenti Pili wito wake mkubwa ni kwa makundi ya wapiganaji na waasi wanawalaza macho raia wa Congo kila uchao. 

“Tunaomba kwa wale watu wenye kufanya fujo au vurugu , tunaowaita waasi tunaomba waache kwa sababu wanaoathirika ni watoto, wanaoathirika ni wamama, wanaoathirika ni watu wazima na sisi katika hayo huwa tunakwenda kujumuika na wakina mama na watoto ambao tunawakuta katika hali zisizoridhisha ambapo watoto wengi huachwa wakiwa yatima. Wanashindwa kuendelea, wanashindwa kusoma na wanashindwa kufanya kitu chochote. Wanatamani sana kuwa kama sisi lakini wanashindwa kutokana na ukosefu wa amani. Hivyo waasi waache vita ili waweze kuishi kwa amani.” 

Na kwa walinda amani wenzie Pili anawapa rai “Tuwasaidie sana akina mama, tuwasaidie sana watoto na waasi waache uvunjifu wa amani kwani hiyo ni chachu ya matatizo mbalimbali katika jamii, watoto wanatamani kutimiza ndoto zao lakini wanashindwa sababu hakuna amani. Tunaiomba dunia na walinda amani wote wasimamie suala la amani ili iweze kurejea na kutawala DRC.”