FIB ya MONUSCO yachukua hatua kuimarisha ulinzi Matembo na Ngadi, DRC

16 Julai 2020

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB, cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, kimefikia makubaliano na wakazi wa kata za Ngadi na Matembo jimboni Kivu Kaskazini ya kutekeleza mradi wa taa za barabarani kama njia mojawapo ya kuimarisha usalama kwenye eneo hilo lililogubikwa na vikundi vilivyojihami vinavyoshambulia raia.

Kikosi hicho cha kujibu mashambulizi kikijumuisha maafisa wa uhusiano kati ya raia na jeshi kutoka nchi tatu za Malawi, Afrika Kusini na Tanzania kimewasili katika kata ya Matembo na Ngadi na kutoa mrejesho wa maombi ya wananchi hao ya ujenzi wa taa za barabarani ikiwa ni sehemu ya kusaidia ulinzi wa raia kwa nyakati za usiku.

Luteni Michael Mudzalimbo kutoka Malawi na anasema kuwa, MONUSCO ilitoa msaada wa fedha kwa ajili ya kusaidia wakazi wa Matembo na Ngadi, mradi huu utasaidia sana kupunguza msongamano barabarani na pia  kuzuia vikundi vya uhalifu dhidi ya wananchi ambavyo vimekuwa vikiwasumbua hasa nyakati za usiku.”

Naye Chifu wa Kata ya Nzuma, Mhindo Kapisa ameshukuru akisema kuwa, “ wanatusaidia kutuletea mwangaza. Nyien yote mnafahama kuwa kama hakuna usalama, na kuna giza unashindwa kufahmu ni vipi utamkimbia adui. Lakini kama kuna mwangaza basi utaweza kumuona adui kwa mbali.  Na hivyo unaweza kukimbia, kwa hiyo kwetu sisi huu ni mpango kamambe sana."

MONUSCO/Force
Hapa ni Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC. Mlinda amani kutoka Tanzania wakati akiwa doriani huko Matembo akisaidia kutibu kidonda raia aliyeumia wakati akilima.

 Wananchi nao wamepaza sauti za shukrani kwa MONUSCO, ambapo mmojawao amesema kuwa“mipangilio ya kuweka taa kwenye mji, tunashukuru sana, na hii isiwe mwisho. Tunaomba muendelee kutusaidia kwa sababu sisi kata mbili ndio kata jirani na MONUSCO na tunashangaa sana wakati mwingine miradi inakwenda kwingine. Lakini tunashukuru kuwa mnaendelea kutukumbuka, kwa hiyo tunaomba msitusahau kwa sababu sisi ni jirani zenu.”

Mkazi mwingine amesema kuwa“tukipata msaada huu tutashukuru sana kwa sababu tutatembeea bila uoga, tutajisikia huru na tutafurahi kabisa. Kwa hiyo msaada ukifika tutasema asanteni sana na Mungu awabariki.”

 Kapteni Yassin Sulemani ni mkuu wa kikundi cha ulinzi hapa na anaelezea vile ambavyo wamekuwa wakiimairisha ulinzi akisema, “dhumuni lililotuleta eneo la Matembo ni kuimarisha ulinzi kwa watu wanaohusika na masuala ya jamii kwa ajili ya kuweka usalama katika maeneo haya na pia kujadiliana mambo mbali mbali yanayohusiana na usalama na yale ya kijamii.”

 Kikosi cha FIB kilianzishwa kwa azimio namba 2098 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 28 mwezi Machi mwaka 2013. Nchi zinazounda kikosi hicho ni Malawi, Afrika Kusini na Tanzania.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter