Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na jamii zinawazowahifadhi Bogo Cameroon wanahitaji kujengewa mnepo:UNHCR

Kijiji cha Tomma Ndjinda kilichokumbwa na mapigano Disemba mwaka jana, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi ziarani.
UN Video
Kijiji cha Tomma Ndjinda kilichokumbwa na mapigano Disemba mwaka jana, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi ziarani.

Wakimbizi na jamii zinawazowahifadhi Bogo Cameroon wanahitaji kujengewa mnepo:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamisha mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi ametoa wito wa msaada na kuwajengea mnepo wakimbizi wa ndani, wakimbizi na jamii zinazowahifadhi katika makazi ya Bogo kwenye jimbo la kaskazini mwa Cameroon. 

Katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Bogo Cameroon Tomma Ndjinda mama wa watoto watano mmoja wa maelfu ya wakimbizi wa ndani kambini hapa akijaribu kuandaa mlo ndani ya hema lake anasema ingawa uhai wa wanawe na wake ulinusurika lakini machafuko yaliyomfungisha virago yalimfanya kupoteza kila kitu.“Nilikuwa nauza sukari, nilikuwa na kila kitu nilichohitaji kwa biashara yangu, na nilipokimbia niliacha kila kitu nilibeba watoto wangu tu. Nilipoona moto unawaka tuliogopa sana na tukakimbia, na kuacha kila kitu. Hivyo tumepoteza kila kitu, mbuzi, kondoo, kuku, na bata”

Machafuko ya kijamii yalizuka mwaka jana baada ya wafugaji na wakulima kupigana wakigombea maji.

UNHCR na washirika wake wanafanya kila wawezalo kutoa msaada wa dharura na kupata suluhu ya muda mrefu katika kuzuia migogoro zaidi na kuleta amani katika jamii hizo za wakulima na wafugaji.

Filippo Grandi amezuru makazi hayo kujionea hali halisi na kusistiza msaada na suluhua ya kudumu ya mgogoro.“Ni lazima tusaidie maridhiano, kwa sababu bila maridhiano na bila ujenzi mpya watu hawatoweza kurejea nyumbani na hiyo itageuka kuwa janga la kibinadamu la muda mrefu lazima tuliepuke hilo. »

Tangu kuzuka kwa machafuko hayo UNHCR inasema takriban watu 100,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani na wengine kukimbilia nchi jirani.

Katika makazi haya ya Bogo ambako UNHCR iliyatengeneza ili kutoa malazi na huduma zingine muhimu wakimbizi wa ndani zaidi ya 2000 wameanza mradi mpya wa kupanda miti ili kulinda mazingira mradi ambao Grandi anasema ni mfano wa kuigwa kwingineko duniani.