Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washambuliaji Cameroon acheni kufanya mashambulizi dhidi ya raia na heshimuni sheria za kimataifa za haki za binadamu-OCHA

Hali ya kukosekana kwa utulivu, imekuwa ikiendelea katika eneo linalotumia lugha ya kiingereza nchini Cameroon
UN OCHA/GILES CLARKE
Hali ya kukosekana kwa utulivu, imekuwa ikiendelea katika eneo linalotumia lugha ya kiingereza nchini Cameroon

Washambuliaji Cameroon acheni kufanya mashambulizi dhidi ya raia na heshimuni sheria za kimataifa za haki za binadamu-OCHA

Amani na Usalama

Taarifa iliyotolewa hii leo na  ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu  masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA, imenukuu ripoti za kuaminika zisemazo kuwa mnamo tarehe 14 mwezi huu wa Februari, watu wenye kujihami kwa silaha waliwaua raia 20 wakiwemo watoto katika Kijiji cha Ntumbo, eneo la Kaskazini Magharibi mwa Cameroon.

Takribani nyumba tisa ziliteketezwa kwa moto katika Kijiji na mashambulizi hayo yamesababisha watu 600 hadi 700 kutawanywa.

Aidha taarifa ya OCHA imeeleza kuwa mnamo tarehe 16 mwezi huu huu wa Februari, kikosi cha msaada wa kibinadamu kilitumwa katika eneo ili kutathimini mahitaji ya wale waliotawanywa. Kutokana na hali mbaya ya usalama, kikosi hicho hakikuweza kufika katika Kijiji cha Ntumbo lakini maafisa waliweza kuzungumza na watu waliopoteza makazi na manusura walikouwa takribani kilomita mbili kutoka kijijini.

Katika maeneo ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon, raia wanabeba mzigo wa ghasia na wanaishi katika hofu. 

OCHA pia imesema kumekuwepo na ripoti za mara kwa mara kuhusu unyanyasaji unatekelezwa na pande zote ikiwemo mauaji, kulindwa kwa watekelezaji wa makossa hayo, utekaji, utesaji na watu kutendewa vibaya, kuteketezwa kwa nyumba na vijiji pamoja na kuvamiwa kwa shule na hospitali. Maafisa wa misaada pia wamekuwa wakitishiwa na kushambuliwa. 

“Tunarejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa, washambuliaji waache kufanya mashambulizi dhidi ya raia na waheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu.” Imesema OCHA

Jumla ya watu milioni 2.3 wako katika uhitaji mkubwa wa chakula, malazi, vitu vingine ambavyo si chakula, pamoja na ulinzi, kwasababu ya mgogoro huo Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon. Idadi hiyo ya watu waliko katika uhitaji, ni sawa na ongezeko la watu milioni moja ikilinganishwa na mwaka uliopita yaani 2019.