Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa COVID-19 lazima kudhibiti ukatili wa kijinsia Cameroon:UNFPA/OCHA

Wala Matari mwenye umri wa miaka 29, aliyewahi kuwa mateka wa magaidi, akiwa kanisani na watoto wake katika kijiji cha Zamai kilichoko kaskazini mwa Cameroon
UN Photo/Eskinder Debebe)
Wala Matari mwenye umri wa miaka 29, aliyewahi kuwa mateka wa magaidi, akiwa kanisani na watoto wake katika kijiji cha Zamai kilichoko kaskazini mwa Cameroon

Wakati wa COVID-19 lazima kudhibiti ukatili wa kijinsia Cameroon:UNFPA/OCHA

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mahitaji ya kibinadamu kwa mwaka 2020 nchini Cameroon yanasalia kuwa makubwa na changamoto inaongezeka kufuatia mlipiko wa virusi vya Corona , COVID-19 hivyo hatua zinahitajika haraka ili kunusuru maisha ya mamilioni ya watu.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA na lile la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, watu milioni 3.9 wanahitaji msaada wa dharura nchini Cameroon kutokana na machafuko ya Boko Haram na vita vilivyozuka nchini humo kutokana na mgogoro wa kisiasa kwenye majimbo ya magharibi na Kaskazini huku hali ikiwa mbaya pia kwa watu wengine zaidi ya 270,000 ambao ni wakimbizi wasiojiweza waliotoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na kuingia kwenye majimbo ya mashriki mwa Cameroon.

Na sasa kutokana na mlipuko wa COVID-19 mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanasema hali imezidi kuwa mbaya kwenye taifa hilo lenye wakimbizi wa ndani 680,000 ambapo asilimia 52 kati yao ni wanawake na watoto.

Yameonya kwamba tathimini iliyofanyika wakati huu wa mlipuko wa Corona imedhihirisha kuwa asilimia kubwa ya mahitaji ya kibinadamu yanaathari za moja kwa moja kwa ulinzi wa wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia GBV, ambao sehemu nyingi duniani pia umeongezeka kutokana na hatua zinazochukuliwa ili kupambana na kusambaa kwa COVID-19 . 

Hivyo mashirika hayo yametoa wito wa msaada wa haraka kuwalinda wanawake na wasichana hao dhidi ya ukatili wa kijinsia, lakini pia kuhakikisha mahitaji mengine ya wakimbizi, wakimbizi wa ndani na jamii zilizotawanywa zinazohitaji ulinzi, malazi, chakula, maji, usafi na huduma za kujisafi, huduma za afya na elimu yanatimizwa.