Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa mafuta ya kisukuku unapeleka kombo malengo ya mabadiliko ya tabianchi:UNEP

ADB/Ariel Javellana
Uzalishaji kutoka kwa mitambo ya kufua umeme wa makaa ya mawe unachangia uchafuzi wa hewa huko Ulaanbaatar, Mongolia.
ADB/Ariel Javellana

Uzalishaji wa mafuta ya kisukuku unapeleka kombo malengo ya mabadiliko ya tabianchi:UNEP

Tabianchi na mazingira

Licha ya kuongezeka kwa matarajio ya mabadiliko ya tabianchi na ahadi za kutokomeza kabisa uzalishaji wa hewa ukaa, serikali bado zina mpango wa kuzalisha zaidi ya mara mbili ya kiwango cha nishati kutoka kwenye mafuta ya kisukuku ifikapo mwaka 2030, kuliko kiwango ambacho kitapunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wa Paris cha nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiasi (1.5° C)

Mafuta ya Kisukuku ni nini?

Mafuta ya kisukuku yanatokana na wanyama na mimea iliyoozea ardhini. Mafuta haya yanapatikana katika gamba la dunia na yanakuwa na hewa za Kaboni na Haidrojeni ambazo zinaweza kuchomwa na kubadilika kuwa nishati. Aina za mafuta ya kisukuku ni pamoja na Makaa ya Mawe, Mafuta kama vile petroli na dizeli pamoja na gesi asilia.

Hiyo ni kwa mujibu wa “Ripoti ya pengo la uzalishaji ya 2021" iliyotolewa leo kwa ushirikiano wa taasisi zinazoongoza za utafiti na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira (UNEP). 

Katika miongo miwili ijayo, ripoti inasema serikali zinakadiria kuongezeka kwa uzalishaji wa mafuta kisukuku na gesi duniani na kupungua kwa kiasi kidogo kwa  uzalishaji wa makaa ya mawe. 

Ikijumuishwa pamoja, mipango hii inamaanisha kuwa kwa ujumla uzalishaji wa mafuta ya kisukuku utaongezeka kwa angalau hadi mwaka 2040. 

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP
UNEP/Natalia Mroz
Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP

Masuala ya haraka 

Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen, "bado kuna wakati wa kupunguza kiwango cha joto na kusalia nyuzi joto 1.5 ° katika kipimo cha Selsiasi kiwango cha juu ya viwango vilivyokuwa kabla ya maendeleo ya viwanda, lakini fursa hii inatoweka haraka." 

Bi Andersen amesema katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26, utakaofanyika mapema Novemba huko Glasgow, "serikali lazima ziongeze hatua, wachukue hatua hizo haraka na kuziba pengo la uzalishaji wa mafuta ya kisukuku na pia kuhakikisha mabadiliko ya haki na ya usawa. Hivi ndivyo tamaa ya kutimiza malengo ya mabadiliko ya tabianchi inavyoonekana.” 

Ripoti ya mwaka huu inatoa wasifu kwa nchi 15 wazalishaji wakuu, ikionesha kuwa nyingi zitaendelea kusaidia kuchangia katika ongezeko la uzalishaji wa mafuta kisukuku. 

Akizungumzia kuhusu ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameangazia matangazo ya hivi karibuni ya nchi za uchumi mkubwa zaidi duniani ya kumaliza ufadhili wa makaa ya mawe, akiyaita kuwa ni "hatua muhimu inayohitajika sana" katika kumaliza uzalishaji wa mafuta kisukuku. 

Kwa António Guterres, hata hivyo, ni kwamba ripoti hiyo inaonyesha kuwa "bado kuna safari ndefu kuelekea siku zijazo za nishati safi." 

"Ni jambo la dharura kwamba wafadhili wote wa umma waliobaki pamoja na mashirika ya fedha kibinafsi, na benki za biashara na mameneja wa mali, wabadilishe ufadhili wao kutoka kwenye makaa ya mawe kwenda kwenye nishati mbadala ili kuachana na hewa ukaa katika sekta ya nishati na kuhakikisha fursa ya upatikanaji wa nishati mbadala kwa wote", ameongeza Guterres. 

Matokeo ya ripoti 

Nchi zilizofanyiwa utafiti zilipanga kuzalisha karibu asilimia 110 ya mafuta zaidi ifikapo mwaka 2030 tofauti na kikomo cha nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiasi, na ni asilimia 45 zaidi ya kile kinachoweza kuruhusu athari ya joto la nyuzi joto 2 katika kipimo cha Selsiasi. 

Ripoti hiyo, iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2019, inapima pengo kati ya mipango ya uzalishaji ya serikali na viwango vinavyoendana na mkataba wa Paris. 

Na miaka miwili baadaye, kiwango cha pengo kimebaki bila kubadilika. 

Mipango ya sasa ingeongoza kwa karibu asilimia 240 ya uzalishaji wa makaa ya mawe, asilimia 57 zaidi ya mafuta kisukuku, na asilimia 71 zaidi ya uzalishaji wa gesi ifikapo mwaka 2030, tofauti na ilivyotakiwa ili kupunguza kiwango cha joto duniani hadi nyuzi joto. 1.5 katika kipimo cha Selsiasi 

Pato la gesi ulimwenguni linakadiriwa kuongezeka zaidi kati ya mwaka 2020 na 2040, ikiwa ni mwendelezo wa mwenendo wa upanuzi wa kimataifa wa uzalishaji wa muda mrefu ambao hauendani na Mkataba wa Paris.

Tangu kuzuka kwa janga la COVID-19, nchi zimeelekeza zaidi ya dola bilioni 300 kwa uzalishaji mpya wa mafuta kisukuku zikiwa ni zaidi zile walizotenga kwa kwa ajili ya nishati safi. 

Kwa upande mwingine, fedha za umma za kimataifa za mafuta kutoka nchi za G20 na benki kuu za maendeleo za kimataifa zimepungua.

Hivi sasa, theluthi moja ya benki hizi na taasisi za fedha za maendeleo za G20 zimepitisha sera ambazo zinaepuka uzalishaji wa mafuta kisukuku siku za usoni. 

Kupunguza lazima kuanze sasa  

Kwa mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, Ploy Achakulwisut, utafiti uko bayana "Uzalishaji wa makaa ya mawe ulimwenguni, mafuta, na gesi lazima uanze kupungua mara moja na kwa kasi ili kuambatana na lengo la muda mrefu la kupunguza ongezeko la joto hadi kufikia nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiasi."

Ripoti hiyo imetolewa na taasisi ya mazingira ya Stockholm (SEI), taasisi ya kimataifa ya maendeleo endelevu (IISD), ODI, E3G, na UNEP. 

Zaidi ya watafiti 80 walichangia uchambuzi na uhakiki, pamoja na vyuo vikuu kadhaa, vituo vya wataalm na mashirika mengine ya utafiti.