Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Video za ubunifu kutoka Syria, Ghana na China zaibuka kidedea shindano la WIPO

Mavuno ya mpunga
Photo: FAO/Olivier Thuillier
Mavuno ya mpunga

Video za ubunifu kutoka Syria, Ghana na China zaibuka kidedea shindano la WIPO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya haki miliki duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la haki miliki, WIPO limetangaza washindi wa shindano la video ya ubunifu kutoka kwa vijana ambapo vijana kutoka Syria, Ghana na China wameibuka kidedea.

Hekma Jabouli kutoka Syria mwenye umri wa miaka 25 aliibuka mshindi wa kwanza kwa video yake inayoonesha kifaa alichobuni nyumbani cha kumwezesha dada yake kuweza kutembea tena baada ya kipande cha bomu kujeruhiwa uti wake wa mgongo.

Nafasi ya pili imekwenda kwa John Wobil kutoka Ghana  ambaye video yake inaonesha kifaa kipya alichobuni cha kupura mpunga shambani.

Kutoka China, vijana wawili wabunifu wa kidijitali Lil Binglu na Cai Quinge ambao wanaishi Japan, wameshika nafasi ya tatu kwa kutengeneza video inayoonesha emoji mpya za kuunganisha watu wanaofanya kazi kutokea majumbani au maeneo ya mbali badala ya kazini.

John Wobil kutoka Ghana amebuni mashine ya kupura mpunga na kusaidia wakulima kuondokana na kupoteza mpunga shambani wakipura kwa mikono- WIPO

Akizugumzia video hizo hii leo katika siku ya hakimiliki duniani iliyobeba maudhui “Hakimiliki na Vijana wabunifu kwa mustakabali bora,” Mkurugenzi Mkuu wa WIPO Daren Tang amesema, nusu ya idadi ya watu duniani wana umri wa chini ya miaka 30 na idadi yao duniani kote inaongezeka kwa kasi.

Amesema “tayari vijana wanafanyia kazi majawabu ya changamoto nyingi zinazotukabili, majawabu ambayo yanaungwa mkono na haki za haki miliki kama vile alama za biashara, hataza na kadhalika kwa lengo la kuwawezesha kupata kipato kutokana na kazi zao hizo.”

Mwaka huu amesema WIPO inasherehekea siku hii kwa kutambua dira na kasi ya wabunifu na wagunduzi vijana kokote kule duniani.

“Katika wakati ambao dunia inapaswa kuja pamoja kushughulikia changamoto lukuki, kuanzia janga la magonjwa na tabianchi, ni lazima tusaidie vijana wetu kufikia uwezo wao wa ubunifu,” amesema Bwana Tang.

Shindano lilifanyika vipi?

Katika shindano hilo, washiriki walitakiwa kuwasilisha video fupi yenye maudhui, “Sisi ni wabunifu vijana. Hebu tujenge mustakabali bora na haki miliki.”
Jumla ya washiriki 142 waliwasilisha kazi zao kutoka mataifa 63 ambapo kundi la majaji lilichagua video 20 kwa kuzingatia vigezo vilivyokuwa vimetajwa.

Video hizo 20 zilipigiwa kura na umma mtandaoni kuanzia tarehe 12 hadi 22 ya mwezi huu wa Aprili ambapo jumla ya kura 36,819 zilipigwa na washindi kuibuka vijana kutoka Syria, Ghana na China.