Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umaskini baado umekita mizizi Ghana licha ya juhudi za kuutokomeza-UN

 Philip Alston, Mwakilishi Maalum kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu.
Picha ya UN /Evan Schneider
Philip Alston, Mwakilishi Maalum kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu.

Umaskini baado umekita mizizi Ghana licha ya juhudi za kuutokomeza-UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Ghana, moja wa nchi za mwanzo kupata Uhuru barani Afrika bado inaghubikwa na umaskini uliokithiri licha ya jitihada za miongo miwili za serikali za kutaka kuutokomeza, amesema mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umasikini uliokithiri na haki za binadamu.

Kutokana na jitihada za serikali ya Ghana kugonga mwamba, Umoja wa Mataifa unatuma mjumbe huko ili kutathmini changamoto zinazoikabili serikali katika jitihada zake.

Mwakilishi huyo , Philip Alston, ataelekea Ghana kutathmini hali ilivyo kwa kutumia jicho la sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu.

Mtalaamu huyo amenukuliwa akisema kuwa, ingawa inatambulika Ghana imepiga hatua katika jitihada za kujaribu  kuutokomeza umaskini katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, hata hivyo, takwimu za serikali zinaonyesha kama umaskini bado upo na pengo la kutokuwepo usawa inaongezeka.

Ameongeza kuwa huu ni wakati mgumu katika historia ya Ghana, kwani mawimbi  yaliyokuwa yanasumbua uchumi wa Ghana kwa kipindi cha  miaka kadhaa nyuma yanaanza kupungua, na kukariri kuwa taifa linahitaji kufuata mkondo wake wa kimaendeleo.

Ameishauri serikali ya Ghana kuhusu umuhimu wa kushughulikia pengo la kutokuwa na usawa katika jamii na kuzifanya haki za binadamu kuwa kitovu cha será zake, endapo wanataka kutimiza malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa hilo .