Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya kaya kwa kaya Kisumu yasaidia kuondoa fikra potofu dhidi ya chanjo

Mhudumu wa kujitolea wa kijamii, CHV Daniel Akothe Awiti akizungumz ana Janet Achieng juu ya umuhimu wa chanjo ya COVID-19 huko Kisumu, Kenya.
UNICEFKenya/LameckOrina
Mhudumu wa kujitolea wa kijamii, CHV Daniel Akothe Awiti akizungumz ana Janet Achieng juu ya umuhimu wa chanjo ya COVID-19 huko Kisumu, Kenya.

Kampeni ya kaya kwa kaya Kisumu yasaidia kuondoa fikra potofu dhidi ya chanjo

Afya

Nchini Kenya harakati za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF za kuondoa fikra potofu katika kaunti ya Kisumu kuhusu chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 zimezaa matunda na sasa hata wale waliokuwa wamesita kupata chanjo hiyo wameanza kupata. 
 

Miongoni mwao ni Ann Otieno, mchuuzi wa maji katika kaunti ya Kisumu nchini Kenya akielezea kuwa awali chanjo ilipoanza kutolewa alikuwa na hofu kubwa kuwa akienda kupata chanjo ataugua na kushindwa kuhudumia watoto wake, kwa kuzingatia anapata kipato kwa kuuza maji.

Kuenea kwa fikra za aina hiyo kulilazimu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Kenya kutumia wafanyakazi wa kujitolea kwenye jamii, CHV kama vile Daniel Akothe Owiti kuelimisha umma umuhimu wa chanjo.

Daniel anasema “kama mhudumu wa kujitolea, naenda kwa familia na kuzungumza nao jinsi ya kujikinga na COVID-19. Pia naziunganisha na vituo ili wapate chanjo”

Janet Achieng, mchuuzi wa mboga Kisumu akafafanua shaka na shuku za awali akisema, “wakati wa mlipuko wa COVID-19 sikutaka kwenda kupata chanjo. Nilikuwa na hofu. Akothe ndio akafika akanitia moyo niende kwa kuwa hakukuwa na ugonjwa. Hata mume wangu alikataa nisiende. Lakini nikaamua kwenda. Niliporudi akaniuliza iwapo najisikia mgonjwa? Nikamwambia, hapana! Niko sawa.”

Ann baada kuelimishwa akachukua hatua akisema, “Daniel alifika na kunishawishi nikapate chanjo kwa sababu ni muhimu kwa wajawazito. Aliniambia itakuwa salama kwangu na kwa mtoto wangu na hata kwa wanangu wengine nikirejea nyumbani.”

Ann alikwenda kituo cha afya na kupatiwa chanjo na sasa anasema anajisikia amepata kinga siyo tu kwake yeye bali pia kwa mtoto wake aliye tumboni.