Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulikuwa tunalala nje sasa msaada wa UNICEF umetuletea faraja- Mkazi Kisumu

Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.
World Bank/Peter Kapuscinski
Mkulima karibu na mji wa Kisumu nchini Kenya akilima shamba lake.

Tulikuwa tunalala nje sasa msaada wa UNICEF umetuletea faraja- Mkazi Kisumu

Msaada wa Kibinadamu

Mvua za kila mwaka katika kaunti ya Kisumu magharibi mwa Kenya huwa ni mwiba kwa wakazi wa eneo hilo kwa sababu huwalaza nje kutokana na mafuriko. Hata hivyo mwaka huu jawabu angalau limepatikana na kuwafuta machozi wakazi 1,900 waliokumbwa na mafuriko ya kati ya mwezi Machi hadi Mei
 

Wakazi wa wilaya za Nyando na Nyakachi jirani na Ziwa Victoria katika kaunti ya Kisumu nchini Kenya,  kando na madhila yatokanayo na mafuriko yasababishwayo na mvua za kila mwaka, maji yanayofurika kutoka ziwani yamekuwa ni mwiba kila uchao. Isaiah Odinga ni mmoja wa manusura wa mafuriko  na  mkazi wa Nyakach.

Bwana Odinga anasema, “wakati mafuriko yamekuja, tulikuwa tumelala usiku na tukashtukia tu maji yameingia kwenye boma yakaharibu kila kitu. Kuku walisombwa na nyumba zilibomoka. Sasa tulipata hasara sana.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake shirika la msalaba mwekundi Kenya na World Vision wakaona shida itokanayo na mafuriko na kuwanyooshea mkono wakazi wa Kisumu.

Bwana Odinga anasema “nimepata msaada nimeshukuru sana. Tumepata blanketi, mkeka, vijiko, sahani na sufuria. Kweli nimeshukuru sana.”

Wakazi hawa pia wanapatiwa fedha taslimu na zina msaada mkubwa ambapo Wangui Karanja, Mkuu wa UNICEF kanda ya Kisumu anasema “fedha zina msaada sana kwa kuwa zinawezesha familia kununua vyakula na vile vile kununua mahitaji mengine ya kaya.”

Kauli hiyo inaungwa mkono na Teresa mchuuzi wa sokoni Nyakach akisema “tunashukuru sana kwa sababu wanatusaidia kuanzisha upya maisha pindi matumaini yetu yalipotoweka. Kwa sababu tunaweza kupika, tuna pahali pa kulala na watoto wetu wanaweza kujifunika kwa blanketi. “

Watu 1,370 katika kaunti ya Kisumu wamepatiwa vifaa vya msaada na UNICEF na mahitaji yao ya muhimu pia yameshughulikiwa.