Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahakikisha huduma ya maji safi na salama yapatikana kwa wanafunzi na wakimbizi Uganda 

Mtoto wa shule akinawa mkono kabla ya kula chakula cha mchono Karenga, Uganda.
© UNICEF/Stuart Tibaweswa
Mtoto wa shule akinawa mkono kabla ya kula chakula cha mchono Karenga, Uganda.

UNICEF yahakikisha huduma ya maji safi na salama yapatikana kwa wanafunzi na wakimbizi Uganda 

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na serikali ya Iceland wanasaidia mradi wa serikali ya Uganda wa kuhakikisha huduma ya maji safi na salama (WASH) inapatikana na kupewa kipaumbele kwa wanafunzi wote kwenye shule za wilaya za Adjumani na Arua nchini Uganda.

Hawa ni baadhi ya wanafunzi katika moja ya shule za msingi kwenye wilaya ya Adjumani nchini Uganda wakiimba kwa furaha wimbo wa kuchagiza usafi wa kunawa mikono kwa maji tiririka safi na salama kwani ni muhimu kwa afya zao. 

 

Kwa mujibu wa UNICEF lengo kuu la mradi huu wa WASH ni kuingilia kati na kutatua changamoto kubwa ya maji katika wila hizo mbili na kuhakikisha kwamba fursa na matumizi ya maji safi na salama ya kunywa na pia huduma za usafi zinawanufaisha idadi kubwa ya wakimbizi katika maeneo hayo lakini pia na jamii za wenyeji zinazowahifadhi. 

Kwa msaada wa fedha zilizotolewa na serkali ya Iceland UNICEF imeweza kuisaidia serikali ya Uganda kujennga matanki makubwa ya maji katika shule 18 za wilaya hizo. 

Ingawa sasa jamii nzima inanufaika na mradi huo lakini walengwa wakubwa ni wanafunzi ambapo 9,400 watafaidika na huduma hiyo ya WASH katika shule mbalimbali za Adjuman na Arua, hatua ambayo UNICEF inasema sio tu itaokoa maisha na kuboresha afya zao bali pia itawapa wanafunzi hao fursa ya kusoma bila hofu ya maradhi yatokanayo na maji kama vile kipindupindu. 

Shirika hilo limeunda kamati maalum katika shule hizo 18 Arua na Adjuman  kuhakikisha usimamizi bora wa miradi hiyo lakini pia imeunda vilabu 18  katika shule hizo ambavyo vimepewa mafunzo ya kuchagiza hulka ya kuzingatia usafi mashuleni.