Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yashtushwa na ongezeko la mashambulizi dhidi ya wakimbizi DRC

Mtoto akiwa katika kami ya wakimizi wa ndani
© UNICEF/Diana Zeyneb Alhindawi
Mtoto akiwa katika kami ya wakimizi wa ndani

UNHCR yashtushwa na ongezeko la mashambulizi dhidi ya wakimbizi DRC

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa linalo hudumia wakimbizi UNHCR na washirika wake wameeleza kushtushwa na ripoti za mashambulizi nane makubwa yaliyotokea katika siku 10 za mwanzo wa mwezi Februari mwaka huu 2022 katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Taarifa kutoka Geneva Uswisi inaeleza kuwa mashambulizi yaliyohusisha watu kuuawa, kutekwa nyara, uporoaji wa mifugo na chakula na kuchoma nyumba moto yamewaathiri zaidi wakimbizi wa ndani. 

Msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amesema shirika hilo limetoa kwa pande zote zinazohusika kusitisha mara moja ghasia dhidi ya raia, wakiwemo waliokimbia makazi yao, ambao wengi wao wamelazimika kukimbia mara kadhaa na hivyo kusababisha rasilimali kuzidiwa uwezo.

“Wimbi la ghasia linafuatia shambulio baya sana lililofanyika tarehe 1 Februari katika eneo la Plaine Savo ambapo ni makazi ya wakimbizi wa ndani, pia katika eneo la Djugu, Ituri. Katika tukio hilo, watu 62 waliuawa na wanamgambo wapiganaji  huku wengine 47 wakijeruhiwa. Hii ilisababisha kuhama kwa watu 25,000 katika eneo hilo, ambao walikimbia kuelekea mji wa Bule ambapo UNHCR na mshirika wake CARITAS wamekuwa wakitoa msaada wa dharura.” Amesem Cheshirkov

Unyama wa makundi ya wanamgambo

Makundi ya wanamgambo katika maeneo ya mashariki mwa DRC yanaendelea kuwalenga raia waliokimbia makazi yao kwa vitendo vya mashamabulizi kuongezeka idadi.

Hivi karibuni(15 Februari 2022) wanamgambo waliwaua watu 17 kwa kuwakata mapanga katika eneo la Lando, Wilaya ya Djugu. Watoto wanane walikuwa miongoni mwa waliouawa. Mama na watoto wake wawili walichomwa moto wakiwa hai huku washambuliaji wakiteketeza nyumba.

Familia za wananchi wa Kongo zikipata hifadhi katika uwanja wa kanisa katoliki huko Drodro, Ituri.
© UNHCR/John Wessels
Familia za wananchi wa Kongo zikipata hifadhi katika uwanja wa kanisa katoliki huko Drodro, Ituri.

Ongezeko la wakimbizi wa ndani

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, mwaka 2016 kulikuwa na wastani wa wakimbizi wa ndani milioni moja huku jumla ya wakimbizi wa ndani milioni 5.6 wakirekodiwa mwishoni mwa 2021.

Usalama wa watoa misaada ya kibinadamu

UNHCR inazitaka pande zote kuruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa msaada kwa wahitaji ili kuokoa maisha yao.

Shirika hilo limesisitiza kuwa matendo ya utekaji nyara na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada, ambayo pia yamekuwa yakiongezeka, lazima yakomeshwe ili waendelee na shughuli zao bila vitisho kwa usalama wao.

Mipango ya UNHCR inahitaji dola milioni 225.4 ili kukidhi mahitaji ya haraka ya waliokimbia makazi yao. Kuendelea kukosekana kwa fedha kwa eneo hilo na DRC kwa ujumla kunazuia utoaji wa msaada unaohitajika.