Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Baba akimuaga mtoto wake wa kiume na familia yake baada ya kuwafikisha eneo salama na kisha yeye kurejea Ukraine

Wakimbizi wa ndani nchini Ukraine wafikia milioni 7.1

© IOM/Francesco Malavolta
Baba akimuaga mtoto wake wa kiume na familia yake baada ya kuwafikisha eneo salama na kisha yeye kurejea Ukraine

Wakimbizi wa ndani nchini Ukraine wafikia milioni 7.1

Amani na Usalama

Vita inayoendelea nchini Ukraine imesababisha zaidi ya watu milioni 7.1 kuyakimbia makazi yao na kusaka maeneo mengine yakuishi ndani ya nchi hiyo ambayo zaidi ya mwezi mmoja imekuwa katika machafuko. 

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM jijini Geneva Uswisi imeeleza hili ni mara ya pili inafanya utafiti wa wakimbizi wa ndani na kwamba idadi hii mpya ni ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na idadi ya mara ya kwanza. 

Mkurugenzi Mkuu wa IOM António Vitorino amesema watu wanaendelea kuyakimbia makazi yao na mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka kwakuwa hawana chakula na wanamahitaji mengine muhimu kama yakujisafi na matibabu. 

“Njia za kupitisha msaada wa kibinadamu zinahitaji haraka kufunguliwa ili kuruhusu watu hawa kupita kwa usalama kwenda kusaka hifadhi katika maeneo salama na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inayohitaja inawafikia kwa haraka ili kuwasadia.”

Ripoti hiyo inaeleza kuwa utafiti uliofanyika kati ya tarehe 24 Machi mpaka tarehe 01 April 2022 imerekodi zaidi ya asilimia 50 ya kaya zina watoto, asilimia 57 zina wazee, na asilimia 30 zina watu wenye magonjwa sugu. 

Wafanyakazi wa IOM hufanya tafiti ili kuelewa vyema safari ya wakimbizi.
© IOM/Monica Chiriac
Wafanyakazi wa IOM hufanya tafiti ili kuelewa vyema safari ya wakimbizi.

Msaada unaotolewa na IOM

Ripoti hiyo imebainisha kuwa zaidi ya theluthi moja ya kaya za wakimbizi wa ndani hawakuwa na kipato katika mwezi uliopita hivyo maisha yao yote yanategemea msaada.

Mkurugenzi Mtendaji wa IOM amesema shirika lake linaendelea kuhimiza kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine ili kurahisisha wananchi kufikishiwa misaada kwa haraka, hata hizo wanaendelea kutoa misaada wa kibinadamu kwa wakimbizi hao katika hali iliyopo sasa.

“Usaidizi wa kifedha, usafiri, chakula, makao, na vitu vya usafi ni miongoni mwa mahitaji makubwa zaidi kwa wakimbizi wa ndani. Pia watu hawa wanahitaji kupatiwa dawa na huduma za afya.” Amebainisha Vitorino.

Usaidizi mwingine ambao tayari umewafikia wananchi  hao ni msaada wa afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia, pamoja na kampeni zinazoendeshwa za kutoa habari za kusaidia kuzuia biashara haramu ya binadamu na unyanyasaji wa kingono na kijinsia.