Mkuu wa UN azuru maeneo yaliyosambaratishwa na vita nje ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv

Mkuu wa UN azuru maeneo yaliyosambaratishwa na vita nje ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko ziarani nchini Ukraine leo Alhamisi, Aprili 28, ametembelea miji ya Irpin, Bucha na Borodyanka na kushuhudia uharibifu mkubwa.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema aliiwazia familia yake katika mojawapo ya nyumba zilizoharibiwa.
"Ninapoona nyumba hizi zimeharibiwa, lazima niseme jinsi ninavyohisi. Nimeiwazia familia yangu katika mojawapo ya nyumba hizo ambazo sasa zimesambaratika na zimetiwa rangi nyeusi. Naona wajukuu zangu wakikimbia kwa hofu, sehemu ya familia hatimaye kufa. Vita hivi ni vya kipuuzi na jinamizi katika karne ya 21. Vita ni mbaya," ameongeza mkuu wa UN huko Borodyanka
Amesisitiza kuwa mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya jinai, ICC tayari anachunguza uhalifu katika miji ya Ukraine, akibainisha kuwa vita yenyewe tayari ni uhalifu.

Katibu Mkuu ametoa rambirambi zake kwa familia za waliopoteza maisha na waliojeruhiwa, akisema, anamtaka kila mtu kutazama pande zote, na kutambua kwamba vita katika karne ya 21 havikubaliki.

Huko Bucha, Guterren alibainisha kuwa uhalifu wa kutisha katika mji huo tayari unachunguzwa na ICC.
"Nimefurahi kwamba mahakama ya kimataifa ya uhalifu inashughulikia suala hili na wawakilishi wa ofisi ya mwendesha mashtaka tayari wamefika hapa," Katibu Mkuu amesisitiza.
Akitangaza kwamba anaunga mkono kazi ya ICC, Guterres ametoa wito kwa Urusi kushirikiana na chombo hiki cha mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kijinai. Wakati huo huo, António Guterres amesisitiza kwamba vita tayari ni uhalifu.
Huko Irpin, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesikitishwa kushuhudia uharibifu mkubwa uliofanyika.

Amesema kuwa raia daima ndio hulipa gharama kubwa zaidi wakati wa vita.
“Raia wasio na hatia waliishi katika nyumba hizi. Wamelipa gharama kubwa zaidi ya vita hivi. Na hii inapaswa kukumbukwa na kila mtu, duniani kote. Popote palipo na vita, gharama ya juu zaidi hulipwa na raia,” ameongeza Bwana Guterres
Mipango ya ziara yake inajumuisha mikutano na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Waziri wa Mambo ya Nje Dmitry Kuleba.

Ikumbukwe kuwa Aprili 26, Guterres alizuru Moscow, Urusi ambako alikutana na Rais Vladimir Putin na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.
Alijadiliana nao, haswa, pendekezo la kuwahamisha watu kwa usalama kutoka Mariupol.
Leo Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Osnat Lubrani, amesema kwamba kwa ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anaondoka kwenda Zaporozhye kujiandaa kwa uwezekano wa uhamisho wa watu kutoka mjini Mariupol.
Ni hali ya kusikitisha na kustaajabisha- Janowski
Naye msemaji wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ukraine Kris Janowski aliyeambatana na Katibu Mkuu katika ziara hiyo nje ya mji mkuu Kyiv amesema "imekuwa ni tukio la kusikitisha na la kushangaza kutembelea maeneo haya, ambayo yameharibiwa sana, na watu wameumizwa na kile kilichowapata. Unaona vijiji, maduka makubwa, mandhari ya kawaida ya miji, iliyovurugwa ghafla na vita, na kumejaa magari yaliyoharibiwa. Kuna dalili zahofu na uharibifu kila kona. Watu wanajaribu kurudi, lakini maeneo yote yanaonekana yako wazi matupu kuliko yalivyokuwa."
Hata hivyo amesema kuna baadhi ya maduka madogo na soko vilivyosalia watu wanastahimili, na maisha yanaanza kurejea taratibu ingawa mustakbali bado haujulikani lakini maisha yanaendelea, na watu wanaendelea na maisha yao.

Maeneo yote yameathirika vibaya
Bwana Jasnowski amesema maeneo yote matatu waliyozuru yameathiriwa vibaya na mashambulizi.
Huko Borodyanka, wamezungumza na gavana wa eneo hilo, ambaye alisema ingawa watu walikuwa wakirudi, bado wanatafuta miili katika baadhi ya nyumba zilizosambaratishwa.
“Unajikuta katika mazingira ya kawaida ya mijini, lakini hujui ni wangapi wamekufa wapendwa wako ni hali ya kutisha sana kwa kila mtu,” amesema Jasnowski
Katibu Mkuu hakupata fursa ya kuzungumza na wakazi wa eneo hilo, lakini alipewa taarifa na mkuu wa wilaya hiyo ya kijeshi wa Borodyanka.
Hata hivyo amesema mkuu wa Umoja wa Mataifa alipata nafasi ya kuzungumza na kasisi wa Kanisa la Orthodoxy huko Bucha, na gavana wa kiraia wa eneo hilo, ambaye alieleza yaliyotukia katika maeneo yao.
“Katibu Mkuu aliguswa sana na aliyoambiwa. Vita ni upuuzi na uhalifu mkubwa . Sisi sote tuna familia, sote tunaweza kufikiria kama hili lingetokea kwa familia zetu wenyewe tungehisi vipi.”
Kwake Janowski anasema “Nilichoshuhudia, kimenirudishia kumbukumbu za wakati nilipofanya kazi na Umoja wa Mataifa Bosnia katika vita vya 1990 wakati wa kuvunjika kwa Yugoslavia.”
Ameongeza kuwa dereva wa Umoja wa Mataifa aliyetupeleka kwenye maeneo hayo matatu pia anatokea Sarajevo, na ilirejesha kumbukumbu zote mbaya kwa wale ambao tulikuwa huko.
“Baada ya vita vya Bosnia na migogoro mbalimbali, sikuwahi kufikiria kwamba ningeona uharibifu wa aina hii ukitokea tena katika maisha yangu, karibu sana na na kitovu cha Ulaya,” amemalizia Janowski.