Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya wananchi wote Afghanistan hawana uhakika wa chakula : FAO

Watu wakisubiri mgao wa chakula kwenye wilaya ya jimboni Herat nchini Afghanistan.
© WFP/Sadeq Naseri
Watu wakisubiri mgao wa chakula kwenye wilaya ya jimboni Herat nchini Afghanistan.

Nusu ya wananchi wote Afghanistan hawana uhakika wa chakula : FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO limesema usaidizi wa muda mfupi na mrefu unahitajika nchini Afghanistan kwa kuwa njaa imesalia katika viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa huku zaidi ya nusu ya watu wote wakiwa hawana uhakika wa chakula.

Zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Afghanistan wanaoishi vijijini ni wakulima na wafugaji. Wananchi hawa kutokana na mzozo wa muda mrefu wamekuwa wakiishi maisha ya kukata tamaa, kaya nyingi zimekuwa zikipata mlo mmoja au miwili kwa siku, kwa kuuza mazao yao au kukopa ilimradi kuhakikisha wana chakula mezani.

Shirika la FAO kwa mwaka huu limedhamiria kuwasaidia wananchi milioni tisa kwa kuwapatia pembejeo za dharura za kilimo, usaidizi wa fedha taslimu na mafunzo ya kiufundi.

Msaada huu unasaidia watu wa vijijini walio katika mazingira magumu kuweza kujitegemea tena kama anavyoeleza Farhad,  mkuu wa familia ya watu saba ambaye ana ng'ombe mmoja, ndama mmoja, na mbuzi watatu aliyepatiwa mbegu za ngano, mbolea na kupatiwa mafunzo ya kiufundi.

“Bila usaidizi tuliopatiwa na FAO tungepoteza mifugo yetu na hali zetu zingekuwa mbaya zaidi. Lakini mbegu za ngano tulizopatiwa zinaonesha matokeo mazuri hadi sasa.”

Maeneo ya vijijini nchini Afghanistan wanawake hawaruhusiwi k​ufanya kazi nje ya nyumba zao. FAO imetengeneza programu maalum za usaidizi kwa wanawake kwa kuzingatia tamaduni zao na Fahima mlezi wa familia ya watu sita anaishukuru FAO kwa jitihada hizo .

Anasema “Tulikuwa tunalima mpunga, lakini kutokana na ukame tulishindwa kulima hivi karibuni. Katika kipindi hiki kigumu, FAO ilitusaidia kwa kutupatia mbegu za soya na mbolea, pia tulipata mafunzo ya upishi wa soya na tukajifunza jinsi ya kupika.”

Wafugaji wengi walio katika mazingira magumu bila usaidizi wa FAO wangeuza mifugo yao kwa kukata tamaa kwa bei ya chini ili waweze kununua chakula na malisho kwa mifugo iliyobaki.

Kwa mujibu wa FAO Afghanistan inahitaji dola bilioni 4.4 kwa ajili ya msaada wa kibinadamu kwa mwaka 2022.