Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa IFAD na Sudan wasuluhisha mzozo kati ya wakulima na wafugaji 

Vituo vya maji kwa ajili ya mifugo vimesaidia kuepusha mizozo kati ya wakulima na wafugaji wanaohamahama.
IFAD Video
Vituo vya maji kwa ajili ya mifugo vimesaidia kuepusha mizozo kati ya wakulima na wafugaji wanaohamahama.

Mradi wa IFAD na Sudan wasuluhisha mzozo kati ya wakulima na wafugaji 

Tabianchi na mazingira

Hatimaye vita vya maji huko Sudan vimepata jawabu ambalo linaonekana la kudumu miongoni mwa wakulima na wafugaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakizozana kila upande ukiona una haki ya kutumia maji ambayo wakati huu yanazidi kupungua kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Jawabu hilo linatokana na mradi  unaotekelezwa kwa pamoja kati ya serikali ya Sudan na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD.

Mradi huo umewezesha ujenzi wa vituo vya kuchota maji ya matumizi kwa binadamu halikadhalika kwa mifugo.

Dkt. Mohammed Ahmed Hassan, Mtaalam wa masuala ya tabianchi IFAD anasema vituo hivyo vya maji kwa ajili ya mifugo vilejengwa kwenye maeneo ambayo ni njia za mifugo hao wakati wa kufuata malisho.

“Tulifanya utafiti wa njia za wanyama ambako huko tulijenga vituo vya maji ya kunywa kwa ajili ya wanyama.

Halikadhalika, IFAD na serikali ya Sudan pia walianzisha na kufadhili kituo cha utatuzi wa mizozo na ujenzi wa amani ambapo mizozo kati ya wakulima na wafugaji inapoibuka, basi hufika kituoni kwa ajili ya mashauriano.

Katika kipindi cha miaka 5 kituo cha aina hiyo kilichoko Kordofan kimetatua zaidi ya mizozo mikubwa 35 ikiwemo katika eneo la Om Rowaba.

Meya wa mji huo Hassan Yaseem  El Hassan ambaye pia ni mshiriki kwenye kituo hicho anasema“tunajaribu kuleta mafanikio kwa pande zote na kufanikisha makubaliano.”

Akilinganisha zamani na sasa, Awdeeyer Abdullah Omer ambaye ni mfugaji anasema “zamani hali ilikuwa ni ngumu. Kabla ya ujenzi wa kituo hiki cha maji, tuliteka maji kutoka kisima kichafu. Wakati mwingine hakuna maji kabisa. Tulilazimika kutembeza punda wetu hadi mbali sana. Lakini sasa tunashukuru kuwepo kwa kituo hiki cha maji.”

Tangu mwaka 2018, mradi huu umewezesha ujenzi wa zaidi ya 190 vituo vya kuhifadhi maji vinavyosaidia zaidi ya kaya 78,000 kwenye eneo hilo la Sudan.

Wafugaji hao wa kuhamahama penginepo watalazimika kuendelea kukabiliana na mabadilliko ya tabianchi, lakini suala la kugombea maji limesalia historia.